MFARANSA, Herve Renard ameteuliwa kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Ivory Cost leo alhamisi, akirithi mikoba ya Sabri Lamouchi aliyejiuzulu baada ya nchi hiyo kutolewa katika hatua ya makundi ya kombe la dunia nchini Brazil.
Renard mwenye miaka 45 alichaguliwa miongoni mwa majina matatu ya mwisho yaliyowajumuisha kocha wa zamani wa Sporting na Benfica, Jose Manuel De Jesus kutoka nchini Ureno na Frederic Antonetti, kocha wa zamani wa timu ya Rennes ya Ufaransa.
Beki huyo wa zamani, aliyeiongoza Zambia kupata ushindi dhidi ya Ivory Coast kwenye mechi ya fainali ya mataifa ya Afrika mwaka 2012 nchini Gabon, amepewa kazi ya kuhakikisha Tembo hao wanafuzu fainali za AFCON 2015 nchini Morocco.
Rais wa chama cha soka nchini Ivory Coast alisema Renard ndiye mwenye mpango mzuri kwa nchi hiyo, na hata mshahara wake aliotaja unalipika, hivyo ndiye aliyestahili.
Renard anakabiliwa na changamoto ya kuitengeneza timu upya baada ya wachezaji wengi kutupwa na umri.
Pia mashabiki na vyombo vya habari vimekuwa vikiiponda timu hiyo, hivyo ni kazi kwake kuiweka sawa.
Kocha huyu amesaini mkataba wa miaka mwiwi ambao unaweza kuongezwa kama atafanya vizuri,na hii kwa mujibu wa rais wa chama cha soka nchini Ivory Coast, Augustin Sidy Diallo.
No comments:
Post a Comment