SIKU Sir Alex Ferguson alipokusanya
virago vyake na Big G zake nyingi ambazo amekuwa akitafuna kwenye benchi la
ufundi la Manchester United na kupanda juu hadi katika bodi, aliondoka siyo tu
na mataji, lakini pia haki ya United kumaliza ‘Top 4’.
Man United wanasikitisha.
Angalia vichapo walivyopata kutoka kwa Manchester City, Liverpool na vibonde West
Brom, walishindwa kabisa kumiliki mpira na hata kwenye sare ya juzi usiku
kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Shakhtar Donetsk, walishindwa kabisa
kufanya mashambulizi ya hatari.
Hata mashabiki wanazi
wa United, wanashindwa kutetea kiwango cha timu yao katika mabishano ya vibanda
umiza; Rio Ferdinand alishindwa kabisa kukaba, Robin van Persie kufunga amesahau
na Ashley Young kusimama tatizo kwake.
Straika aliyekuwa
akililia kuondoka, Wayne Rooney ndiye pekee anaonyesha kiwango cha mchezaji wa
dunia kwa sasa katika kikosi cha Man United, nashindwa kujua na yeye angeondoka
ingekuwa vipi?
Na hawa ndiyo wachezaji
wale wale ambao walikuwa hawakamatiki msimu uliopita na walishinda ligi
kirahisi. Unajua kwanini? Ferguson alikuwa bonge la kocha kuwahi kufundisha
Ligi Kuu England. Cha kusikitisha Moyes hajamfikia hata kidogo, siyo kwamba ni
kocha mbaya, ni tu hajafika ‘levo’ za Fergie.
Ni mara ngapi, Moyes
ameshinda ugenini dhidi ya timu za ‘top 4’, alipokuwa Everton?
Hakuwa na kipindi
kizuri cha kiangazi. Alimsajili, Marouane Fellaini kucheza sambamba na Michael
Carrick kati kati. Fellaini alionyesha kiwango kizuri Everton akicheza nyuma ya
straika na alifiti kwenye mfumo wa soka la moja kwa moja lililojaa krosi ambalo
lilifundishwa na Moyes.
Akiwa kama kiungo hana
kasi, ananguvu, lakini hapendi kukaba kwa nguvu, stamina hana na siyo fundi,
wala mjanja mjanja na hana tofauti na Carrick. Siyo kosa la Moyes kumleta pale,
hii inatokana na kwamba alimsajili kutokana na presha ya kukosa wachezaji
aliokuwa akiwataka.
United wanakosa ubunifu,
kitu ambacho Moyes alijaribu kukitatua wakati wa kiangazi kwa kutaka kuwasajili
kina Thiago Alcantara, Cesc Fabregas. Bahati mbaya kwake hakuna aliyetaka kutua
Old Trafford.
Hatahivyo, kuna swali
linazuka kwanini Shinji Kagawa hachezeshwi katika nafasi iliyomfanya kuonekana
kama mmoja kati ya viungo bora duniani pindi alipokuwa Borussia Dortmund?
Hutakiwi kujibu swali
hili ambalo limekuwa likiulizwa kila kukicha. Kagawa alikuwa moyo wa Dortmund
wakati wakianza kupanda na kutawala Ulaya.
Hakutakuwa na tatizo
lolote kumsogeza Rooney mbele acheze kama mshambuliaji nafasi ambayo anaipenda
sana na kumpanga Kagawa nyuma yake sehemu ambayo ilimfanya Fergie amuone na
kumsajili kutoka Dortmund. Badala ya kuwatumia Danny Welbeck na mzee wa
kujiangusha Ashley Young kwenye timu.
Kuiponda United kwa
sasa hivi ni kitu rahisi sana, kwa sababu huitaji ‘degree’ ya ukocha kuona
makosa kibao ya Moyes katika kikosi cha Man United, lakini kumshambulia siyo
lengo la makala haya.
Lengo kuu ni kuonyesha
kwamba kikosi chake siyo kikali na hakijawa kikali kwa miaka kadhaa iliyopita
tangu enzi zile za utatu mtakatifu wa Rooney, Carlos Tevez na Cristiano Ronaldo
ambao kila aliyepita mbele yao ilikuwa kiama.
Ferguson alikuwa
anaijua sana kazi yake na kuwafanya United mabingwa hata walipokuwa na timu
mbovu. Naweza kusema kwamba kama, Fergie angepewa kufundisha Everton, wangekuwa
miongoni mwa timu tishio England na kutoa upinzani kwenye ubingwa.
Hatahivyo, ukiiangalia
ligi ilivyo msimu huu, Man City na Chelsea wanavikosi vikubwa zaidi, Arsenal
wanakocha bora na Tottenham Hotspur bahati iko kwao na Liverpool timu
walishaijenga msimu uliopita.
Kuwa huru kubishana na
ukweli huu, lakini nionavyo, United hawatakuwa mabingwa, washindi wa pili,
washindi watatu au wanne wala watano, watamaliza ligi kwenye nafasi ya sita,
yangu mimi ni hayo tu.
No comments:
Post a Comment