Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Tuesday, August 20, 2013

LIGI KUU NDIO HIYO INAANZA ILA KOMBINESHENI YA SIMBA MBELE BADO, MASHABIKI WAWE WAVUMILIVU



USHINDI wa mabao 4-1 ya Simba waliyoifunga Sports Club Villa ya Uganda kwenye mchezo wa maadhimisho ya tamasha la Simba Day, linalofanyika kila mwaka huwezi kusema kuwa ni kipimo cha Simba kufanya vizuri kwenye Ligi Kuu Tanzania bara inayotarajiwa kuanza Agosti 24, mwaka huu.

Mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ulihudhuriwa na mashabiki wengi wa Simba pia watani wao wa jadi wakiwepo kujionea uhondo wa siku hiyo maalum kwa watani wao uliosindikizwa na wasanii wa muziki wa kizazi kipya.

Simba ambayo iliialika SC Villa kwa ajili ya kunogesha sherehe hizo, ambazo zinafanyika kwa mwaka wa tano sasa ilianza kwa kuwatambulisha wachezaji wake wote waliosajiliwa kwa msimu wa 2013/14 akiwepo mshambuliaji Mrisho Ngassa ambaye pia amesajiliwa na Yanga.

Mashabiki wa Simba waliondoka uwanjani wakiwa na furaha baada ya ushindi wa mabao 4-1 ambao Wekundu hao waliupata na kufanya wengine wakidiriki kusukuma Vogue ya mshambuliaji Betram Mwombeki ambaye alifunga mabao mawili peke yake kwenye mchezo huo. 

Simba kipindi cha kwanza walicheza mchezo ambao ulikuwa hauna ladha huku wachezaji wake wakitoa pasi ambazo hazina macho (hazifiki kwa mlengwa) na kuwafanya Sports Club Villa kuwashambulia na kufanikiwa kupata bao rahisi  dakika ya tisa ya mchezo, kupitia kwa Mganga Robert, ambaye alimalizia krosi ya Sijali Jamal kwani mabeki wa Simba walimfuata Jamal na kumsahau Robert.

Simba dakika 45 za kipindi cha kwanza haikufanya mashambilizi ya kutisha kiasi cha kusema kuwa kombinesheni iliyoanza inaweza kuwa kikosi cha kwanza japo ilikuwa na wakongwe kipa Abel Dhaira, Nassor Massoud, “Cholo”, Ramadhan Chombo “Redondo” Amri Kiemba, Jonas Mkude, Abdulmalik Humud aliyesajiliwa toka Azam FC na Betram Mwombeki.

Kutokana na kikosi cha Simba kutoelewana kuanzia safu ya ushambuliaji kilikosa magoli mengi kwani walikuwa wakishambulia toka nyuma wakifika kiwanja cha wapinzani karibu na goli wanarudisha mashambulizi nyuma na kuwafanya kuanza upya.

Pia kuna uchoyo wa pasi pale wanapokuwa karibu na goli, hii sishangai kwani baadhi ya wachezaji wetu wanapenda waonekane ndio wamefunga wakisahau kuwa mchezo wa soka ni wa kusaidia na ndio maana wapo 11 uwanjani na kila mtu ana dakika nne za kuuchezea mpira.

Bao la Simba la kusawazisha ambalo walilipata dakika ya 43, kupitia kwa Jonas Mkude, ambaye aliachia  shuti akiwa nje ya eneo la penati, lilipita katikati ya mabeki wa Sports Club Villa na kujaa moja kwa moja wavuni na kufanya matokeo kuwa 1-1 na kwenda mapumziko wakiwa wameshusha presha lilikuwa juhudi binafsi baada ya kuona wanapoa pasi mbele lakini ama zinakwenda nje au kuishia mikononi mwa golikipa.

 Kipindi cha pili Simba ilibadilika na kuanza kushambulia  baada ya kufanyika mabadiliko kadhaa ya kuwatoa Ramadhan Chombo na nafasi yake kuchukuliwa na Wiliam Lucian, Joseph Owino na kuingia Hassan Isihaka na Amri Kiemba akaingia Abdallah Seseme na kufanya mchezo kubadilika.

Kikosi cha wachezaji chipukizi waliokuwepo awali na waliosajiliwa msimu huu ndicho kilichoonyesha mchezo wa kuvutia na kushambulia kwa nguvu muda wote na kuwafanya mashabiki kushangilia muda wote wa kipindi cha pili.

Kuingia kwa Wiliam Lucian kulifanya mchezo uonekane wenye ladha kwani alikuwa akisaidiwa mashambulizi na beki kinda Issa Rashid  maarufu kama “Baba Ubaya” ambaye ana uwezo wa kupanda na kushuka kutokana na mbio alizonazo na uwezo wa mapafu yake.
             
Simba imejitahidi kufanya usajili mzuri kwa wachezaji chipukizi  lakini kwa Abdulhalim Humud na golikipa Andrew Ntalla unaweza kusema imepotea kwani uchezaji wao hauna tija kwa timu. Pia mshambuliaji Betram Mwombeki  anahitaji kupata mchezaji ambaye ana uwezo wa kumlisha mipira kwani anaweza kuwamudu mabeki  na kuwa “goal getter”  kwa vile mwili wake ulivyojengeka kiuchezaji ukinakshiwa na urefu wake.

Simba mwishoni ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Mwombeki na nafasi yake kuchukua Ramadhani Singano 'Messi' na Marcel Kaheza akamrithi Haroun Chanongo walicheza kandanda safi lakini bado kocha Abdallah  Kibaden anakazi ya kurekebisha kikosi chake ili kicheze kitimu na kufanya mashambulizi yanayofika mwisho siyo timu ifanye shambulizi ikifika karibu na eneo la penalti inarudisha mpira kwenye kiwanja chake.

Kwa vile soka ni mchezo wa kupokezana na ndio maana wana kuwa 11 uwanjani  wachezaji wanatakiwa wasiwe wachoyo kupeana pasi pindi anapoona yeye hayupo kwenye nafasi nzuri ya kufunga kuliko kupiga ili uonekane bora umepiga.

Pia mashabiki wakubali kuwa timu inavyocheza michezo mingi ndivyo wachezaji wanavyozidi kuzoeana na kucheza vizuri hivyo mashabiki wanatakiwa kukubaliana na matokeo yoyote kwa kipindi cha mwanzo hasa kwa kikosi kilichobadilika kama cha Simba.
                                                                                              


No comments:

Post a Comment