SIMBA SPORTS CLUB
15/04/2013
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
KLABU ya Simba inapenda kutoa taarifa zifuatazo kwa vyombo
vya habari siku ya leo, Jumatatu, Aprili 15, 2013.
KUHUSU TIMU
MARA baada ya mechi ya jana dhidi ya Azam FC, wachezaji wote
wa Simba walipewa mapumziko ya siku mbili (leo na kesho) na timu itaanza tena
mazoezi keshokutwa Jumatano asubuhi katika viwanja vya Leaders, Kinondoni
jijini Dar es Salaam .
Wachezaji wamepewa mapumziko hayo kutokana na kutumika kwa
kipindi kirefu mfululizo tangu timu ilipokwenda katika mikoa ya kanda ya ziwa
na kambini Bamba Beach jijini Dar es Salaam.
Ni matarajio ya uongozi na benchi la ufundi kwamba wachezaji
hao wataanza mazoezi wakiwa na nguvu mpya na tayari kwa changamoto ya mechi nne
zilizobaki kumalizia Ligi Kuu ya Tanzania .
Uongozi wa Simba unawaomba wapenzi na wanachama wake
kuendelea kuisapoti timu yao
kwa namna ileile waliyoionyesha katika mikoa ya kanda ya ziwa na dhidi ya Azam
jana. Ingawa uwezekano wa kutwaa ubingwa haupo wala kutwaa nafasi ya pili,
lakini bado kuna kazi ya kutetea heshima na hadhi ya Simba ili iweze kumaliza
katika nafasi nzuri.
Wachezaji na viongozi hawataweza kufanya lolote pasipo umoja
na mshikamano wa wapenzi na wanachama wake. Kama
kauli mbiu ya Simba isemavyo, “NGUVU MOJA.”
MECHI YA AZAM
PAMOJA na kukubaliana na matokeo ya mechi ya jana dhidi ya
Azam, uongozi wa Simba unapenda kuweka rekodi wazi kwamba haukuridhishwa na
uchezeshaji wa mwamuzi, Oden Mbaga, hasahasa katika kipindi cha pili.
Kwa bahati nzuri, msimamo huu wa Simba hauna hata chembe ya
ushabiki kwa vile hata washabiki waliokuwa katika upande wa watani wetu wa
jadi, nao pia walionekana kutofurahishwa na uchezeshaji wa Mbaga.
Mbaga ni mwamuzi mwenye beji ya Shirikisho la Soka Duniani
(FIFA) na katika hali ya kawaida ilitazamiwa mechi ingechezeshwa kwa viwango
vya kimataifa lakini hali ilikuwa kinyume chake.
Simba inaamini kwamba Mbaga hakuutendea haki mchezo ule wa
jana. Simba inasema hivi kwa sababu inataka mwamuzi huyo ajirekebishe na kwamba
matokeo ya mechi viwanjani yaamuliwe na ubora wa timu na si maamuzi yenye
utata.
UJUMBE MFUPI WA
MANENO KWENYE SIMU (SMS)
KUNA ujumbe mfupi wa maneno umeenezwa kwenye baadhi ya simu
za mkononi za wapenzi wa Simba zikidai kwamba washabiki wa Yanga waliokuwa
wakiishangilia klabu yetu jana walifanya hivyo kwa sababu klabu hizi mbili
zimeingia katika mahusiano.
Ujumbe huo ukadai kwamba lengo la mahusiano hayo mapya baina
ya Simba na Yanga ni kuhakikisha kwamba Simba inafungwa kwa idadi kubwa ya
mabao kwenye mechi ya watani wa jadi Mei 18 mwaka huu.
Ujumbe huo, ukaenda mbali zaidi kwa kudai kwamba hata kambi
ya Simba ya Bamba
Beach imefadhiliwa na
Yanga.
Ujumbe huo wa simu ni wa kuchekesha. Na unachekesha sana . Yeyote aliyetunga
meseji hii ana nia ya kuleta machafuko ndani ya klabu ya Simba. Inaonekana
haridhishwi na hali ya amani iliyopo klabuni kwa sasa.
Uongozi wa Simba unakana kuwepo kwa mahusiano yoyote ya
kuhujumu timu baina ya viongozi wa klabu na Yanga. Kitendo cha kushangiliwa kwa
timu pinzani si kigeni kwani kimewahi pia kutokea katika nchi kadhaa duniani.
Ikumbukwe kwamba kimsingi, si jinai au mwiko kwa shabiki wa
Yanga kuishangilia Simba. Kama washabiki wa
wapinzani wetu wa jadi walivutiwa na kiwango chetu na kuamua kutushangilia,
hiyo haikuwa dhambi.
Uongozi unapenda kuwaomba wanachama wa Simba kuwa na imani
na uongozi wao na kufahamu kwamba unafanya kila unaloweza kulinda na kuhifadhi
hadhi na heshima ya klabu.
Imetolewa na
Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
Simba SC
No comments:
Post a Comment