ROGASIAN Kaijage ameteuliwa kuwa kocha mpya wa
timu ya taifa ya mpira wa miguu ya wanawake, Twiga Stars baada ya kocha wa
zamani, Charles Boniface Mkwasa kujiuzulu katikati ya mwaka jana.
Mkwasa, ambaye alikuwa nyota wa Yanga na Taifa
Stars, alijiengua kufundisha timu hiyo aliyoiongoza kwa muda mrefu, baada ya
Twiga Stars kuondolewa katika kinyang’anyiro cha kuwania tiketi ya kucheza
fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) zilizofanyika nchini Equatorial
Guinea.
Twiga ilipata bao muhimu la ugenini jijini
Addis Ababa ilipofungwa na wenyeji wao Ethiopia mabao 2-1, lakini ikiwa na
matumaini ya kutumia vyema bao la ugenini ilijikuta ikilala bao 1-0 kwenye
Uwanja wa Taifa katika mchezo wa marudiano na hivyo kukosa tiketi ya kurudi tena
kwenye fainali hizo.
Kaijage ambaye kwa sasa anajihusisha na mradi
wa vijana (grassroots) pamoja na programu nyingine za kukuza vipaji zilizo chini
ya TFF, aliteuliwa na Kamati ya Ufundi ya TFF kufanya kazi hiyo na ameita kikosi
cha Twiga Stars kwa mazoezi ya siku kumi kuanzia Machi 10 hadi 23 mwaka huu
Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
Wachezaji walioitwa ni Amina Ally (Lord
Barden), Asha Rashid (Mburahati Queens), Aziza Mwadini (Zanzibar), Esther
Chabruma (Sayari), Esther Mayalla (TSC Academy), Etoe Mlenzi (JKT), Evelyn
Sekikubo (Mbarahati Queens), Fatuma Bushiri (Simba Queens), Fatuma Mustafa
(Sayari) na Fatuma Omari (Sayari).
Flora
Kayanda (Tanzanite), Hamisa Athuman (Marsh Academy), Hellen Maduka (Bujora),
Hellen Peter (JKT), Irene Ndibalema (TSC Academy), Maimuna Said (JKT), Mwajuma
Abdallah (Tanzanite), Mwanaidi Tamba (Mburahati Queens), Mwanahamis Omari
(Mburahati Queens) na Mwapewa Mtumwa (Sayari).
Nabila Ahmed
(Marsh Academy), Nasiria Hashim (Zanzibar), Pulkeria Charaji (Sayari), Rukia
Khamis (Sayari), Semeni Abeid (Tanzanite), Sharida Boniface (Makongo Sekondari),
Sophia Mwasikili (Luleburgaz Gucu Spor, Uturuki), Theresa Yona (TSC Academy),
Vumilia Maarifa (Evergreen) na Zena Khamis (Mburahati
Queens).
No comments:
Post a Comment