Licha ya kuanzisha mashindano ya kombe la Meya lenye lengo la kujenga mahusiano mazuri kati ya halmashauri ya manispaa ya Tabora na wananchi lakini halmashauri hiyo imeshindwa kutoa hata kiasi kidogo cha fedha kama zawadi kwa washindi wa mashindano hayo yaliyozishirikisha zaidi ya timu 18 za manispaa ya Tabora.
Katika mashindano hayo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Vita mjini Tabora yalikuwa na wakati mgumu kwa kile kilichodaiwa kuwa kukumbwa na ukata katika uendeshaji wa ligi hiyo.
Katibu wa Chama cha soka manispaa ya Tabora TUFA, Juma Mapunda amedai kuwa pamoja na jitihada kadhaa za kufuatilia na kuomba msaada kwa halmashauri ya manispaa ya Tabora lakini hakuna kiongozi yeyote aliyeonesha hali ya kutaka kusaidia mashindano hayo.
Mapunda alisema hata hivyo uongozi wa TUFA unafikiria namna ya kuacha kuendesha mashindano hayo ya kombe la Meya kwani hakuna sababu ya kuendelea nalo huku wahusika(uongozi wa halmashauri) wakionesha kutojali.
Kwa upande wa mgeni rasmi katika fainali ya mashindano hayo ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa miguu mkoa wa Tabora Yusuph Kitumbo alisema kuna haja ya kuwakutanisha wadau wa soka na kuwahamasisha umuhimu wa soka na hasa kwa wakati huu wa kutafuta vipaji vya vijana.
Alisema ni aibu kwa halmashauri kuyatelekeza mashindano hayo ya kombe la Meya wakati wao kama taasisi ya serikali ndio iliyoanzisha na kutambua umuhimu wa michezo hiyo.
Kitumbo ambaye ndiye aliyeamua kutoa zawadi za fedha kwa mshindi wa kwanza timu ya Reli Tabora ilijipatia kiasi cha shilingi elfu 75 wakati mshindi wa pili ikijipatia kiasi cha shilingi elfu 50 fedha ambazo Kitumbo alidai kuwa hazijakidhi mahitaji ya zawadi kwa wachezaji wa timu hizo.
No comments:
Post a Comment