Kamati ya Utendaji ya
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, imeteua Kamati ya Rufaa ya Leseni za
Klabu, ikiwa ni maandalizi ya kuanza msimu mpya wa mashindano ya soka
yanayosimamiwa na kuendeshwa na TFF.
Viongozi na wajumbe waliteuliwa
na kupitishwa Jumapili Julai 30, 2017 katika Mkutano wa Kamati ya Utendaji
uliofanyika Ukumbi wa Hosteli za TFF, zilizopo Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume,
Ilala jijini Dar es Salaam yaliko Makao Makuu ya shirikisho.
Viongozi na Wajumbe
walioteuliwa ni Msomi Wakili Dk. Damas Ndumbaro atayekuwa Mwenyekiti; Msomi
Wakili Alex Mngongolwa (Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo) wakati Wajumbe ni
Meneja wa zamani wa Uwanja wa Taifa, Charles Matoke, Tumainiel Mlango na Ahmed
Menye.
Viongozi wa Kamati hiyo
watakuwa na majukumu ya kusililiza rufaa kutokana na uamuzi wa Kamati ya Leseni
za Klabu inayoongozwa na Msomi Wakili Lloyd Nchunga ambayo inasimamia
utekelezaji wa Kanuni ya 11 ya Ligi Kuu.
Kwa mujibu wa kanuni hiyo ya
11, Klabu za Ligi Kuu zinawajibika na kutakiwa kuwasilisha maombi ya kupatiwa
Leseni ya Klabu kwa TFF katika muda utakaotangazwa na Kamati ya Utendaji ya TFF
na kuhakikisha zinakidhi masharti na vigezo vyote vya msingi kupatiwa leseni
ili kuweza kushiriki Ligi Kuu.
Kanuni hiyo ya 11 inasema
kwamba Klabu itakayoshindwa kukidhi kiasi cha kukosa Leseni haitashiriki Ligi
Kuu kwa msimu husika. Vigezo hitajika kwenye kupata leseni ya klabu ni kuwa na
Uwanja wa nyumbani wa mechi, uwanja wa mazoezi, umiliki wa klabu moja, kuwa na
timu ya vijana, uwepo wa ofisi rasmi na watendaji wake akiwamo mtendaji mkuu
(CEO) na maofisa masoko, habari na mhasibu mwenye taaluma ya uhasibu.
Tayari Klabu zilielekezwa
kuwasiliana na Meneja wa Leseni za Klabu, Jemedari Said ambaye ni Ofisa
Maendeleo ya Mpira wa Miguu Tanzania wa TFF kwa ajili ya maelezo ya kuchukua na
kurejesha fomu kwa mujibu wa taratibu na kanuni za mashindano kabla ya kuanza
rasmi mashindano.
No comments:
Post a Comment