Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Sunday, April 30, 2017

DK. MAKOYE APANIA MAKUBWA TaSUBa









 Wadenishi waahidi kuendelea kusaidia vifaa vya muziki kwa ajili ya kufundishia na kujifunzia; Tamasha la Bagamoyo lawavuta wengi.
Na Rahel Pallangyo
TAASISI ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) ni miongoni mwa taasisi tatu za Tanzania ziliteuliwa kuwa vituo vyenye ubora uliotukuka (Centres of Excellence) kwenye maeneo yake ya msingi.
TaSUBa iliteuliwa kuwa kituo cha ubora uliotukuka kwenye ufundishaji katika nyanja za utamaduni na sanaa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (East African Community Centre of Excellence in Culture and the Arts).
Malengo mahsusi ya TaSUBa kuwa kituo cha ubora uliotukuka ni pamoja na kuendesha mafunzo ya sanaa na utamaduni kwa wasanii wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, kukuza sanaa na utafiti kwenye eneo la utamaduni, kuzishauri nchi zinazounda Jumuiya ya Afrika Mashariki katika maeneo ya uhifadhi, ukuzaji na maendeleo ya sanaa na utamaduni na kuratibu na kuendesha tamasha la Sanaa na Utamaduni kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Historia ya TaSUBa
TaSUBa ni Wakala wa serikali iliyoanzishwa kwa mujibu wa sheria ya Wakala wa Serikali Na. 30 ya mwaka 1997 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2009, kupitia tangazo la  Serikali Na. 220 la Novemba 2, 2007.

Taasisi hii inatokana na kilichokuwa Chuo cha Sanaa Bagamoyo ambacho kilianzishwa mwaka 1981 baada ya kuvunjwa kwa kikundi cha Sanaa za Maonyesho cha Taifa mwaka 1980.
Baada ya kuundwa kwa Wizara ya Utamaduni mwaka 1962, kilianzishwa kikundi cha Sanaa za Maonyesho cha Taifa ambacho kilianza na fani ya ngoma (1963), Sarakasi (1969) na Tamthilia (1974). 
Kazi kubwa ya Kikundi hiki ilikuwa kufanya maonyesho sehemu mbali mbali nchini ili kukuza mwamko wa kuupenda na kuutukuza utamaduni wa Watanzania ambao mkoloni alijitahidi kwa nguvu zake zote kuukandamiza.
Kazi za kikundi hicho ni kuwahamasisha Watanzania wajivunie utamaduni wao na washiriki kikamilifu kuufufua, kuukuza na kuulinda.  Makazi ya Kikundi yalikuwa Shariff Shamba- Ilala, Dar es Salaam, mahali zilipo ofisi za Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).
Mtendaji Mkuu wa TaSUBa, Dk Herbert Makoye wamejipanga kuhakikisha Taasisi hiyo inakuwa kituo cha mafunzo ya Sanaa na Utamaduni chenye ubora uliotukuka barani Afrika.
Malengo ya TaSUBa
“Kwa sasa TaSUBa ni kituo bora uliotukuka kwa Afrika Mashariki hivyo tumejiandaa kuhakikisha tunakuwa bora Afrika nzima na kwa sasa inawezekana kwani serikali ya Denmark imetupatia vifaa vya kufundishia na kujifunza vyenye thamani ya milioni 100 na serikali pia imetupatia shilingi milioni 100 tukanunulia vifaa,” alisema Dk. Makoye.
Pia Dk. Makoye alisema wamedhamiria kuzalisha wasanii, viongozi wa sanaa na wafanyakazi katika sekta ya utamaduni sambamba na kuzalisha kazi za sanaa pamoja na huduma za multimedia.
Dk. Makoye alisema kwa upande wa wafanyakazi na waalimu wamejipanga kuandaa wakuzaji wa sanaa, wasanii, waendeshaji na wasimamizi wa shughuli za sanaa kwenye sekta za umma na binafsi. Kwa sababu sanaa na utamaduni kwa kiasi kikubwa unaanza kupotea pia wanaandaa watafiti na washauri wa sanaa na utamaduni kwa ngazi ya taifa na kimataifa.
Kukuza viwango vya sanaa na moyo wa kupenda mila na desturi za Mtanzania na kukuza mwamko wa matumizi ya sanaa katika mapambano ya matatizo mbalimbali katika jamaii.
Shughuli za TaSUBa
Taasisi inatoa mafunzo katika nyanja za Ngoma, Maigizo, Muziki, Sarakasi, Sanaa za ufundi, Ufundi wa Majukwaa, Sayansi ya jamii (Uongozi na Utawala wa masuala ya sanaa, TEHEMA, Ujasiliamali, Haki Miliki, Kiswahili na Kiingereza
Pia katika Ubunifu na uzalishaji wa picha jongefu, ubunifu na uzalishaji wa muziki na sauti.
Katika kuhakikisha malengo waliojiwekea yanatimia Mtendaji Mkuu wa TaSUBa Dk. Makoye alisema kwa mwaka huu wanatarajia kutumia tamasha la Bagamoyo kujitangaza kimataifa hasa nchi za Afrika Mashariki na Afrika nzima.
Dk. Makoye alisema tamasha la Bagamoyo linatarajiwa kufanyika Septemba 23-30 mwaka huu kwenye viwanja vya Taasisi hiyo huku likipambwa na vyakula vya aina mbalimbali vya asili, ngoma za asili, nguo za asili na vitu vingine vya asili ya hapa Tanzania.
“Tunatarajia kutumia Tamasha la Bagamoyo kuitangaza TaSUBa kwenye nchi za Afrika Mashiriki kwani kwenye nchi za Ulaya tunafahamika na watu wanakuja kusoma hapa,” alisema Dk. Makoye.
Pia Makoye alisema tayari nchi za Denmark, Norway na China zimeshathibitisha kushiriki tamasha la mwaka huu ambalo ni la 35 tangu kuanza mwaka 1991.
Aidha Dk. Makoye alisema lengo la kujitangaza kwenye nchi za Afrika Mashariki ni kuwavutiwa kuja kusoma na kujifunza utamaduni kwenye taasisi hiyo ambayo ni kituo bora katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Nayo serikali ya Denmark katika kuhakikisha TSUBa inatoa mafunzo kwa vitendo imetoa msaada wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia muziki yenye thamani ya shilingi milioni 100.
Balozi wa Denmark, Einar Jensen wakati akikabidhi vifaa hivyo alisema Tanzania na Denmark wana ushirikiano wa miaka 50 sasa na wamekuwa wakishirikiana katika kuendeleza utamaduni na Sanaa katika jamii za watanzania na kuahidi kuendelea kusaidia.
“Muziki ni njia mojawapo ya kusaidia kufikisha ujumbe na huwezi kufanya hivyo bila kutumia vifaa ndio maana Denmark tumeona umuhimu wa kusaidia nyanja hii,” alisema Jensen.
Dk. Makoye,  alisema msaada wa vifaa hivyo vya Wadenish utasaidia kuboresha mafunzo ya muziki yanayotolewa na TaSuBa na kuahidi kuvitunza na kuvilinda ili viweze kutimiza lengo la kununuliwa kwake.
“Vifaa hivi vimekuja wakati muafaka kwa sababu Taasisi ipo kwenye harakati za kuimarisha programu zake ikiwa ni pamoja na kuongeza udahili ili vijana wengi wa Kitanzania ili wapate fursa ya mafunzo,” alisema Dk. Makoye.
Pia Dk. Makoye alisema vifaa hivyo vitasaidia eneo la upigaji wa muziki kuondoa malalamiko yanaelekezwa kwa wasanii wengi wa muziki kuwa hawana uwezo wa kutumia au kupiga vyombo vya muziki wanapokuwa wanatumbuiza.
Aidha Dk. Makoye alisema Denmark imekuwa ikisaidia TaSUBa katika kuimarisha taaluma kwani mwaka 2016 ilitoa msaada wa vyombo vya muziki pamoja na komputa na makabati ya kutunzia vifaa hivyo vya muziki.
Mwaka 1994 ubalozi wa Denmark uligharamia uendeshaji wa Sanaa shirikishi kwa kushirikiana na TaSUBa  kwenye jamii za wilaya ya Bagamoyo na udhamini wa uchapishaji wa kitabu cha Sanaa na maendeleo kilichoandikwa na Juma Bakari na Ghonche Materego ambao walikuwa wafanyakazi wa taasisi hiyo.

TaSUBa inatoa kozi ya Astashahada mwaka mmoja, katika masomo ya yafuatazo:
Katika Sanaa za Maonyesho na Sanaa za Ufundi, katika Teknolojia na Ubunifu wa Sauti na Muziki, katika Uzalishaji wa Filamu na Vipindi vya Television.
Pia Stashahada  miaka miwili kwenye masomo yafuatazo:
Katika Sanaa za Maonyesho na Sanaa za Ufundi, katika Teknolojia na Ubunifu wa Sauti na Muziki na katika Uzalishaji wa Filamu na Vipindi vya Television
Pia TaSUBa inatoa kozi fupi fupi ambazo zinaandaliwa kulingana na mahitaji maalum ya walengwa ambazo zinafundishwa kwenye maeneo yote ya taaluma zinazotolewa na TaSUBa
ambazo ni Utunzi muziki, uimbaji, upigaji wa ala mbalimbali za muziki, teknolojia ya muziki na ngoma.
Uigizaji wa michezo ya kuigiza na filamu, uandishi wa miswada ya michezo ya kuigiza na filamu, uongozaji wa michezo ya kuigiza na filamu, ubunifu wa malebo, ufundi wa jukwaa, sarakasi, uchoraji, graphic design, uhariri wa filamu na upigaji wa filamu.
Dk. Makoye anawaalika watu, makampuni na taasisi zinazohusu sanaa na utamaduni kujiunga na TaSUBa ili wapate mafunzo katika kozi ambazo watachagua wenyewe na kuacha kufanya kazi bila kusoma kwa kisingizio cha uzoefu.

No comments:

Post a Comment