NYOTA ya
mshambuliaji wa Simba, Mrundi Laudit Mavugo imezidi kung’ara baada ya leo
kuifungia timu yake bao pekee na kuipeleka robo fainali ya michuano ya Kombe la
Shirikisho (FA) kwa kuifunga African Lyon bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa Dar es
Salaam.
Hiyo ni
mechi ya tatu mfululizo kwa mshambuliaji huyo kufunga kwenye michuano yote
inayoshiriki Simba, baada ya kufunga bao moja katika kila mechi dhidi ya
Majimaji na Prisons.
Iliichukua
dakika 58 kwa Mavugo kufunga bao hilo baada ya kuunganisha pasi nzuri ya Saidi
Ndemla kabla ya kuujaza mpira nyavuni.
Simba
ilicheza vizuri katika mechi hiyo na ilianza kwa kulishambulia lango la
wapinzani wao tangu mwanzo wa mchezo.
Dakika ya
16, Mavugo alipoteza nafasi ya kufunga kabla ya Juma Luizio kukosa nafasi
nyingine baada ya shuti lake kupanguliwa na kipa wa Lyon Rostand Youthe.
Dakika ya
32, Ibrahim Ajibu alipoteza nafasi nyingine ya kufunga baada ya shuti lake
kupaa juu ya lango akiwa yeye na kipa.
Katika
kipindi cha pili,Simba ilifanya mabadiliko kwa kuwatoa Luizio na Ndemla na
nafasi zao kuchukuliwa na Shiza Kichuya na Mohamed ‘Mo’ Ibrahim.
Hata baada
ya mabadiliko hayo, Simba haikumudu kuongeza bao kwani Lyon walionekana
wakicheza kwa tahadhari kubwa kuepuka kufungwa mabao mengi.
Simba na
Lyon zimekutana kwa mara ya pili msimu huu, mara ya kwanza ilikuwa kwenye mechi
ya Ligi Kuu ambapo Simba ilifungwa bao 1-0 na Lyon kwenye uwanja wa Uhuru Dar
es Salaam.
Simba:
Daniel Agyei, Janvier Bokungu, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Abdi Banda, Jonas
Mkude, Novaty Lufunga, James Kotei, Said Ndemla/Mohammed ‘Mo’ Ibrahim dk70,
Laudit Mavugo/Pastory Athanas dk85, Ibrahim Ajibu na Juma Luizio/Shiza Kichuya
dk59.
African
Lyon: Rostand Youthe, Miraji Adam, Baraka Jaffary, Omary Salum, Hamad Waziri,
Hassan Isihaka, Peter Mwalyanzi, Hamad Manzi/Awadh Juma dk49, Rehani Kibingu,
Venance Joseph na Omary Daga/Fred Cosmas dk72.
No comments:
Post a Comment