Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Saturday, January 14, 2017

Man United vs Liverpool ni patashika leo



*Ndio watani wa jadi hasa England tangu zama
*Mtihani mwingine kwa Mourinho na Jurgen Klopp
*Ni wakati wa kubadili mbinu dimbani Old Trafford


UKISIKIA utani wa jadi wa soka katika Uingereza, kwa asili ni huu
baina ya Manchester United ‘Mashetani Wekundu’ na Liverpool ‘The
Reds’.

Katika taifa hili hawa ndio walikuwa wakubwa enzi hizo, wakitambiana
kona zote na wakiwa na ushindani mkubwa hasa.

Hawa ni kama Simba na Yanga nyumbani Tanzania, na unaposikia au kusoma
juu ya utani wa jadi au uhasimu wa soka mwingine, ni wa maeneo tu,
kama London (Chelsea vs Arsenal), London Kaskazini (Arsenal vs
Tottenham Hotspur), Greater Manchester (Manchester City vs Manchester
United) au Merseyside (Everton vs Liverpool). Hatuwezi kusahau kule
Kusini Cardiff vs Swansea.

Wa Man United dhidi ya Liverpool ni uhasimu wa miaka mingi na hapana
ubishi kwamba ya leo ni ‘Big Match’ yaani ‘Mechi Kubwa’.

Old Trafford, ngome ya miaka mingi ya United ambayo ilikuwa vigumu
kuivunja ndipo kipute kinapigwa.

Hii ni mechi ya 50 kwa Liverpool kukutana na United kwenye Ligi Kuu ya
England (EPL). Liver wamekuwa wazuri, lakini katika wiki za karibuni
United nao wametokea kuchanua, wakielewana na kucheza kitimu wakipata
ushindi.

Hali hii ndiyo inauweka mtiti huu katika mvutano mkubwa. The Reds
wamefurahia, hadi leo asubuhi, ushindi wa mechi tisa mfululizo chini
ya Jurgen Klopp, sita kati ya hizo zikiwa ni za EPL.

Ushindi huo umewasaidia kupanda ngazi hadi nafasi ya pili kwenye
jedwali la msimamo wa ligi. Atakayeshinda mechi ya leo anaeweza
kufikiriwa zaidi juu ya uwezekano wa kushindana kiukweli kuuendea
ubingwa.

Jose Mourinho na tambo zake ana kazi nzito, maana Liver hujipanga hasa
na hakuna ubishi kwamba tunashuhudia mengi, ndani na nje ya dimba
kutoka kwa makocha na hata wachezaji, achilia mbali washabiki.

United wapo kwenye kiwango cha juu kwa sasa wakiwa na akina Paul Pogba
na Zlatan Ibrahimovic wanaotarajiwa kucheza leo.

Chelsea wanaongoza lakini mserereko wao wa kushinda mechi 13 mfululizo
ulitulizwa na Spurs waliowapiga 2-0 katika mechi ya EPL.

Kwa kawaida msimu wa sikukuu na Januari huweza kuwa mpindo kwa baadhi
ya timu. Liver ambao walianza vyema tangu mwanzo wa msimu kwa
kuwakandamiza Arsenal, wanajulikana kwa shinikizo zao tangu mechi
inapoanza.

Hata hivyo, wameshikisha breki majuzi kwa kupigwa na Bournemouth kabla
ya kwenda sare na Sunderland huku kwenye nusu fainali ya EFL
wakifungwa na Southampton.

Kwenye mechi ya Kombe la FA dhidi ya Plymouth walishikwa pia, wakaishia na sare.
Matokeo ya leo Old Trafford – yawe chanya, hasi au kati yatakuwa na
athari kubwa kwa klabu zote.

Iwapo Wayne Rooney atacheza anaweza kuvunja rekodi na kuwa mwanasoka
aliyefunga mabao mengi zaidi katika historia ya klabu hiyo.
Akifanya hivyo dhidi ya Liverpool ataona fahari kubwa sana, na wenzake
pamoja naye.

Kwa sasa amefungana ka mabao na Sir Bobby Charlton aliyeshikilia
rekodi hiyo kwa muda mrefu, akiwa na mabao 249. Rooney alimfikia
wikiendi iliyopita alipofunga bao la kwanza dhidi ya Reading kwenye
mechi ya Kombe la FA.

Kwake anaweza kuwa na mambo mengi sana kichwani kwa hili, japokuwa
wengine wanaliona ni dogo; tilia pia maanani mshambuliaji huyu alikuwa
mwaminifu kabisa kwa Everton (mahasimu wa Liverpool mahalia) na sasa
anacheza dhidi ya mahasimu hao ngazi ya taifa.

Uhasama wa Liverpool na United unachangiwa, pamoja na mambo mengine,
miji mikubwa wanakotoka timu hizi, kwani ndiyo majiji makubwa ya hapa
England – Liverpool na Manchester yakitanguliwa na London.

Historia ya uchumi wao na mchuano wa kiviwanda unachangia kwa kiasi
kikubwa kuupa utamu utani wao huu.

Hizi ni timu kubwa kwa hakika, zikiwa zimepata heshima ndani na nje ya
nchi, ikiwa ni pamoja na kupata ubingwa nyumbani na Ulaya na kuwa na
washabiki wengi hata ng’ambo,

Ukiwachanganya kwa pamoja wamepata kutwaa makombe 38 ya ligi hapa
nyumbani, manane ya Ulaya, matatu ya Uefa, moja la Kombe la Dunia la
Klabu, moja la Intercontinental Cup na 36 ya FA kwa Ngao ya Jamii.

Timu hizi kijiografia zipo umbali wa maili 35 na tangu wakati ule wa
mapinduzi ya viwanda pamekuwapo msuguano na utani baina yao kuhusiana
na masuala ua uchumi na viwanda, kila mji ukijidai kwamba upo juu ya
mwingine.

Katika karne ya 18 Manchester ilikuwa juu zaidi na kuonekana kama
ndiyo kioo cha ukanda wa Kaskazini lakini Liverpool hawakuwa wakipenda
hilo.

Kwa upande mwingine ni kwamba Liverpool ilikua moja ya miji mikubwa ya
bandari huku kukiwa na ukuaji wa masuala ya viwanda vya nguo.

Kutokea kwa Vita ya I ya Dunia kulivuruga soka ya hapa nyumbani,
ambapo mashindano yalianza tena 1919 ambapo Liverpool walikuwa juu
huku United wakishuka na kuja kushushwa daraja 1923 na kuwa huko chini
kwa misimu mitatu.

Wakati Man U wakipata uthabiti mwaka 1947, Liverpool walishuka daraja
huku United wakiwa chini ya nahodha wa zamani wa Liverpoo, Matt Busby,
na kutwaa Kombe la FA 1948.

Kuna utata katika kuchagua wachezaji; Ibrahimovic alikosa mechi ya
nusu fainali ya kwanza ya Kombe la EFL dhidi ya Hull kutokana na
ugonjwa lakini Mourinho amekuwa na imani kwamba Mswidi huyu atarejea.

Bosi huyo anaweza kuwakosa mabeki wawili wa kati. Eric Bailly anakuwa
ng’ambo kuwakilisha Ivory Coast kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika
(AFCON) nchini Gabon.

Marcos Rojo anauguza majeraha aliyopata wikiendi iliyopita kwenye
mechi ya Kombe la FA na hakuwa ikijulikana kama hadi leo angekuwa
timamu kushuka dimbani.

Klopp yeye ana tatizo pia, kwani mshambuliaji wake tegemeo, Sadio Mane
naye amejiunga AFCON huko Gabon kuwakilisha Senegal. Mjerumani huyu,
hata hivyo, anajipa moyo kwa kurejea kwa Philippe Countinho.

Huenda leo makocha wakabadili mbinu. Kwenye mechi iliyopita, Oktoba
mwaka jana, walikwenda suluhu, ambapo Mourinho alieleza kufurahia
walivyoidhibiti Anfield na kubadili hali ya hewa uwanjani hapo.

Lakini hayo yalikuwa mwaka jana, si mwaka huu. Muda umebadilika na
Reds ni tofauti kwani wachezaji wamezoea zaidi maelekezo na mbinu za
kocha wao.

Bila shaka mechi itakuwa tamu, wanakocheza si Anfield, ni Old
Trafford, ni Mancheter, ni United, dimba lipo tayari kwa mechi kubwa.

Cio…

No comments:

Post a Comment