Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Monday, January 16, 2017

SIMBU AWAGARAGAZA WAKENYA MUMBAI MARATHON



 
MWANARIADHA Mtanzania Alphonce Simbu, ameibuka mshindi wa mbio ndefu za Mumbai Marathon ya mwaka huu huku akimpiku Mkenya Joshua Kipkorir pamoja na wakimbiaji wengine wazoefu kutoka mabara mbalimbali.

Mashindano hayo yanayojulikana kama Standard Chartered Mumbai Marathon huwa yanafanyika kila Jumapili ya tatu ya Januari katika Jiji la Mumbai, India na yanaaminika kuwa ni mbio kubwa kabisa barani Asia kwa idadi ya washiriki wanaomaliza mbio hizo.

Simbu, ambaye anadhaminiwa na kampuni ya Multichoice Tanzania, aliibuka mshindi kwa kutumia muda wa dakika 2:09:28 muda ambao ni mzuri kwa mbio za aina hiyo.

Akizungumzia ushindi wake, Simbu alisema kuwa anaamini ushindi huo umesababishwa na maandalizi aliyoyafanya na
anauchukulia ushindi huo kama changamoto kwa mashindano mengine makubwa na kwamba huo ni mwanzo tu.

"Ushindi huu si wangu mwenyewe bali ni ushindi wa Taifa zima la Tanzania, pia huu utanipa hamasa kujituma zaidi kwenye mashindano mengine makubwa," alisema Simbu.

Kwa upande wa Serikali, Waziri wa Habari, Utamaduni , Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alimpongeza kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter akisema; "Tumefanikiwa tena, hongera Simbu, hongera RT (Chama cha Riadha Tanzania), asanteni Multichoice Tanzania kwa kumsapoti. Mungu ibariki Tanzania,".

Naye Mkuu wa Mahusiano wa Multichoice Tanzania, Johnson Mshana alisema; "Multichoice imefurahishwa sana na matokeo hayo, tulichukuwa jukumu la kumdhamini Simbi katika mazoezi na maandalizi yake kwa kipindi cha mwaka mzima, kwani tunafahamu fika kuwa mazoezi na maandalizi ndiyo siri kubwa ya mafanikio katika mchezo wowote.

“Dhamira yetu kubwa ni kuinua vipaji na kulirejesha taifa letu kwenye ramani ya dunia katika ulingo wa michezo na burudani," alisema Mshana.

Katika mbio hizo, waigizaji maarufu wa Bollywood, John Abraham na Neha Dhupia walikuwepo kuleta amsha amsha kwa washiriki. Simba anatarajia kurejea nchini kesho Jumatatu.

No comments:

Post a Comment