Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Saturday, January 14, 2017

Wanasoka waliowachefua wanazi



'TUNAKUCHUKIA kupita kiasi, maana tulikupenda mno' ni moja ya mabango

yaliyopata kushikwa na washabiki wa soka, ambao huwaambii lolote kwa
klabu wanayoipenda, na hupanda wazimu mchezaji nyota anapowakimbia
kwenda kwa wapinzani wao.

Ingekuwa ni ndani ya uwezo wao, wanazi hao wangewaadhibu wachezaji na
kuhakikisha ama hawachezei mahasimu wao au wanafanya vibaya, lakini
kwa vile majaliwa ni ya Rabuka, washabiki huishia kuzomea, kuandika
mabango na kujaribu kuwachanganya wachezaji hao wanapokabiliana na
timu zao dimbani.

Wayne Rooney aliyepasuana kichwa na kocha Alex Ferguson Manchester
United akililia kuhama, alianzia makali yake Everton chini ya kocha
aliyekuja kumfuata United, David Moyes.

Ni ajabu kwamba wakati Moyes anawasili Old Trafford, alilikuta jalada
la Rooney mezani kwake, akiomba kuhama, naye akamkatalia na hadi leo
ni nahodha wa Mashetani Wekundu Hao.

Rooney alianzia timu ya vijana ya Everton, akacheza chini ya kocha
huyo Mskochi huyo, lakini uhusiano wao uliharibika, Moyes akimsanifu
Rooney kwamba anakula kupita kiasi na hata alipohamia United 2004
Moyes hakujali, lakini washabiki waliona wamesalitiwa.

Baadaye Moyes alimshitaki Rooney kwa fidia ya dola milioni 7.5 kwa kumkandia kwenye
kitabu cha wasifu wake. Rooney anadai Moyes alivujisha mazungumzo yao
wawili walipokutana Liverpool Echo. Watakaaje Old Trafford leo kama
kocha na mchezaji?

Sol Campbell aliwatapisha nyongo washabiki wa Tottenham Hotspurs
alipoamua kuhamia kwa mahasimu wao wa London Kaskazini huko, Arsenal
mwaka 2001. Washabiki wa Spurs walimfyonya na kumwelezea kuwa
amechina.

Campbell aliondoka akiwa nyota na nahodha wa Spurs, akawa mchezaji wa
kwanza mwenye nafasi hizo kuhama, tena kwenda kwa mahasimu wao.

Kilichowaumiza zaidi wanazi wa White Hart Lane, ni ukweli kwamba
Arsenal walimchukua kama mchezaji huru, hawakuwalipa hata ndururu.

Tabia chafu ya baadhi ya washabiki wa Spurs ya kumtishia maisha
ilimsababisha Campbell kuajiri baunsa na kutembea naye karibu kila
mahali.

Zlatan Ibrahimovic wa Manchester United alishaingia Arsenal, lakini
Arsene Wenger alipotaka kwanza amjaribu, ngongoti huyo akatimka mchana
kweupe, alitaka mkataba bila kujaribiwa. Alishapewa kabisa fulana
iliyoandikwa jina lake pale Highbury – uwanja wa zamani wa Arsenal
kabla hawajahamia Emirates.

Ibrahimovich baadaye alikuja kuwachefua washabiki wa Juventus
alipoamua kuondoka klabuni hapo na kujiunga Inter Milan - zote za Ligi
Kuu ya Italia.

Kipande hicho cha mtu kimekuwa kikiitwa msafiri asiyefika, kwani
hajawahi kukaa zaidi ya miaka mitatu kwenye klabu moja.

Alikuwa mmoja wa nyota wa Juventus kati ya 2004 na 2006, hasa
alipoanza kuwika kwenye ligi, ambapo alifunga mabao 16 kwenye Serie A.
Kashfa ya Calciopoli (ya upangaji matokeo) iliwasababisha Juventus
kushushwa daraja hadi Serie B, ambapo mastaa kadhaa, kama Alessandro
Del Piero, David Trezeguet na Pavel Nedved waliapa kubaki na timu ili
kuisaidia kurudi Serie A, lakini Zlatan akataka afunguliwe mlango.

Alitishia kuwashitaki, na hatimaye akajiunga na wapinzani wao, Milan,
na ndipo waumini wa Juventus walipopoteza kabisa imani naye. Leo yupo
Man United.

Utasemaje kuhusu Ashley Cole kuwaacha Arsenal na kwenda Chelsea?
Amejipalia mkaa, na hadi leo ni mmoja wa wachezaji ambao mashabiki wa
Arsenal wanawachukia zaidi. Wanazi hawakuona sababu ya yeye kuhama na
kujiunga na watani zao wa London, wakasema ni uchu uliokithiri wa
fedha.

Siku chache kabla ya kuondoka Arsenal, Cole alisema: "Naipenda klabu
hii lakini nahisi kuna baadhi ya watu humu humu klabuni wasiotaka
kuniona nikiendelea kuvaa jezi ya The Gunners. Sitakaa nijisajili
klabu nyingine yoyote ya Ligi Kuu, maana sitaweza kabisa kucheza dhidi
ya Arsenal, labda nikacheze ng'ambo."

Wiki moja tu baada ya maneno hayo kumtoka, yaani mwaka 2006, Roman
Abramovich alituma watu wake, mshahara ukaongezwa mara dufu na kufikia
dola 135,828, tamaa ikamwaka akala matapishi yake na kukimbilia
Stamford Bridge.

Kuna timu zilitambiana sana, na John Robertson alijikuta katikati yao,
nazo ni Nottingham Forest na Derby County, ambapo winga huyo mjanja
alikuwa shujaa wa Nottingham. Akiwa na hesabu sahihi za kumimina
majalo, Robertson alikuwa kwenye kikosi cha kocha Brian Clough
kilichotwaa Kombe la Ulaya mfululizo mwaka 1979 na 1980.

Lakini watu wake walinuna 1983, alipofanya uhamisho tata kwenda Derby
County, na huko aliungana na msaidizi wa zamani wa Clough, Peter
Taylor, kitu kilichojenga chuki ya aina yake kati ya marafiki hao
wawili wa zamani. Robertson alikuwa sababu ya wawili hao kutozungumza
tena daima. ITAENDELEA.

Cio…

No comments:

Post a Comment