Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Wednesday, December 21, 2016

AZAM FC KUANZA RAUNDI YA KWANZA KOMBE LA SHIRIKISHO BARANI AFRIKAWAKATI Azam FC, wakiwa safarini Ruvuma kucheza na Majimaji kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, habari njema kwao wamepangwa kuazia hatua ya kwanza kwenye kombe la Shirikisho barani Afrika.
Azam FC itaanza kucheza nyumbani  na mshindi kati ya Opara United ya Botswana na  Mbabane Swallows ya Swaziland wakati KVZ ya Zanzibar itaanzia hatua ya awali nyumbani kwa kucheza na Messager Ngozi ya Burundi.
Mashindano yaliyopita Azam FC iliandika rekodi ya kuwa timu pekee ya Afrika Mashariki kuanzia raundi ya kwanza kwenye michuano hiyo na hata kwa wale walishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, zingine zote za ukanda huo zilianzia raundi ya awali.
Azam FC kwenye raundi ya kwanza ilikutana na Bidvest Wits ya Afrika Kusini na kuitoa kwa jumla ya mabao 7-3, ikiwafunga ugenini mabao 3-0 na kuwapa kipigo kingine cha nyumbani 4-3.
Raundi ya pili mabingwa hao wakakutana na vigogo wa Tunisia, Esperance na kujikuta ikifa kiume kwa kutolewa kwa jumla ya mabao 4-2.
CAF msimu huu imebadilisha mfumo wa mashindano hayo, ambapo imepanua wigo kwa timu zitakazoingia hatua ya makundi kutoka nane hadi 16, kila michuano itahusisha makundi manne yenye timu nne kila moja.
Mfumo huo unamaanisha kuwa timu 32 zitakazocheza raundi ya kwanza inayofuata baada ya ile ya awali kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, zile 16 bora zitakazoshinda zitaingia moja kwa moja katika hatua ya mwisho ya mtoano (play off).
Katika hatua hiyo zitakutanishwa na timu nyingine 16 zilizotolewa katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, na wale 16 bora watakaopenya hapo watafuzu moja kwa moja kwenye hatua ya makundi, itakayoanza kuchezwa Mei mwakani.
Pia CAF imepandisha zawadi kwa washindi wa Kombe la Shirikisho, wakati bingwa akivuna Dola za Kimarekani Milioni 1.25 (sawa na zaidi ya Bilioni 2.72 za Kitanzania), mshindi wa pili atajizolea Dola za Kimarekani 625,000 (sawa na zaidi ya Sh. Bilioni 1.36).
Timu zitakazoingia nusu fainali kila mmoja itajizolea Dola za Kimarekani 450,000 (sawa na zaidi ya Sh. Milioni 979.96), zilizoingia robo fainali nazo zitazoa Dola za Kimarekani 350,000 (sawa na zaidi ya Sh. Milioni 762.19) huku zile zitakazoshika nafasi ya tatu na nne kwenye makundi zikiambulia Dola za Kimarekani 275,000 (sawa na zaidi ya Sh. Milioni 598.86).