Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Friday, May 13, 2016

YANGA KUKABIDHIWA KOMBE KESHO NA WAZIRI MWIGULU



YANGA inashuka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kesho kupambana na Ndanda FC katika mechi ya duru la pili Ligi Kuu Tanzania Bara inayofikia tamati Mei 22 mwaka huu.
Yanga inayonolewa na Mholanzi Hans Pluijm, itashuka dimbani ikiwa tayari imetetea ubingwa wake, ikiwa inaushikilia kwa mwaka wa pili mfululizo, ambapo leo mchezo huo utatumika kuikabidhi kombe lao.
Msimu uliopita wa ligi hiyo, Yanga ilitwaa ubingwa wakiwa na mechi mbili mkononi, lakini safari hii wamechukua wakiwa na mechi tatu.
Hiyo inatokana na Simba kufungwa bao 1-0 na Mwadui FC Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kitendo ambacho kiliisafishia njia Yanga kabla, kwani kulikuwa hakuna timu ambayo ingepata pointi 69 za Yanga. Simba ingekuwa ikishinda mechi zake zilizobaki ingefikisha pointi 67.
Lakini Yanga iliupamba maua ubingwa huo Jumanne baada ya kuifunga Mbeya City mabao 2-0 na kufikisha pointi 71, ambazo hakuna timu ya kuzifikia.
Yanga itaingia uwanjani leo, ikicheza kwa tahadhari kubwa kuhofia kupata majeruhi, kwani Jumatano ijayo, inakabiliwa na mchezo mgumu dhidi ya Esperanca ya Angola katika michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF CC).
Mara ya mwisho Yanga ilipocheza na Ndanda FC, Yanga ilipata ushindi mwembamba wa bao 1-0, lililofungwa na beki Kelvini Yondani.
Kwa mazingira, ni wazi Ndanda hawatokubali kupoteza mchezo wa pili mbele ya timu hiyo, ambayo leo itakabidhiwa kombe lake la ubingwa.
Pluijm aliliambia gazeti hili kuwa licha ya kutumia mchezo wa leo kama maandalizi yake ya  mwisho kabla ya kuivaa Esperanca, anaupa umuhimu mkubwa na wachezaji wake hawatabweteka katika mechi zote zilizosalia.
 “Sijawahi kuidharau timu yoyote inayocheza Ligi Kuu, iwe ipo juu katika msimamo au inapigana kukwepa kushuka daraja, nimebakiwa na mechi mbili, mfumo wangu ni ule ule wa kushambulia na kufunga magoli mengi, kila timu nitahakikisha naifunga kwa idadi kubwa ya mabao,” alisema Pluijm.
Kwa upande wa kocha wa Ndanda, Abdul Mingange alisema kikosi chake ambacho ni wenyeji wa mchezo huo watahakikisha wanapata ushindi na kujiweka vizuri zaidi. Ndanda inashika nafasi ya 10 katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 33.
Rekodi ya ubingwa Yanga
Yanga imefanikiwa kutwaa ubingwa wa 26 mwaka huu, ubingwa ambao tangu kuanzishwa kwa Ligi Kuu Tanzania Bara hakuna timu yoyote iliyofikia idadi hiyo.
Simba ya Dar es Salaam yenye upinzani na Yanga inashika nafasi ya pili ikiwa imetwaa mara 18. 
 Tambwe avunja rekodi
Mrundi Amissi Tambwe amefunga mabao 21 hadi sasa katika ligi hiyo na kuvunja rekodi ya Abdallah Juma aliyefunga mabao hayo 20 ndani ya kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Rekodi ya kufunga mabao mengi inashikiliwa na Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ aliyefunga mabao 24 katika ligi hiyo mwaka 1994.
Tambwe pia ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa kigeni nchini kufunga zaidi ya mabao 20 katika ligi Tanzania.
Pia ameweka rekodi mpya ya kuwa mchezaji mwenye mabao mengi zaidi Ligi Kuu Tanzania Bara ndani ya kipindi cha misimu mitatu tu baada ya kufunga mabao 54.

No comments:

Post a Comment