NI zaidi ya ubingwa, ni zaidi ya sherehe; ndicho unachoweza kusema baada ya Yanga kunogesha 'pati lao' la
kutwaa taji la 24 la Ligi Kuu Bara kufunga msimu na ushindi safi katika mchezo dhidi ya mahasimu wao uliofanyika jana kwenye Uwanja wa wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga, ambayo tayari ilishatangazwa kuwa mabingwa wa msimu
huu wa Ligi Kuu, ilinogesha sherehe zake za kukabidhiwa taji hilo katika mchezo
wa mwisho ambao waliweza kuibamiza Simba mabao 2-0 na kuweza kutimiza furaha
yao ya kunyakua ubingwa huku wakiwanyuka mahasimu wao hao.
Kutokana na ushindi huo, Yanga sasa imefunga msimu huu kwa
kukusanya pointi 60, pointi nane zaidi ya Azam FC kwenye nafasi ya pili na
pointi 15 zaidi ya mahasimu wao hao, Simba, ambao wamemaliza ligi kwenye nafasi
ya tatu.
Mchezo huo uliovutia mashabiki wengi kutoka pande zote za
nchi hiyo na kuchezeshwa na mwamuzi, Martin Saanya kutoka Morogoro, Yanga
iliweza kufungua akaunti yake ya mabao mapema katika dakika ya tano tu kupitia
Didier Kavumbangu, aliyefunga kwa kichwa baada ya kona iliyopigwa kwenye lango
la Simba lililokuwa likilindwa na Juma Kaseja.
Bao hilo liliweza kudumu hadi mapumziko, ambapo vijana hao
wa Mholanzi, Ernie Brandts waliokuwa wameweka kambi yao visiwani Pemba walikwenda
kwenye vyumba vya kubadilishia nguo wakiwa mbele kwa bao hilo 1-0.
Baada ya kuingia kwa bao hilo, Simba ilipata nafasi ya
kusawazisha katika kipindi hicho cha kwanza baada ya kupata penalti, lakini
ilishindwa kutumia faida hiyo.
Ilikuwa katika dakika 27, ambapo winga hatari Mrisho Ngassa
alichezewa madhambi na kuangushwa ndani ya boksi na beki Nadir Haroub
'Cannavaro' na kumfanya mwamuzi Saanya kuamuru ipigwe penalti, ambapo Mussa
Mudde alishindwa kutumia faida hiyo kwa kumpiga mkwaju huo mikononi mwa kipa wa
Yanga, Ally Mustafa ‘Barthez’ na kuudaka.
Kukosa penalti hiyo kuliishusha ari kidogo Simba, licha ya
kushuhudia wakipoteza nafasi kadha za kufunga, huku ukuta wa Yanga uliokuwa
ukiongozwa na Cannavaro na Kelvin Yondani, Mbuyu Twite na David Luhende kufanya
kazi kubwa ya kumlinda kipa wao, Barthez.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Yanga waliendelea
kulisakama goli la wapinzani wao Simba na hatimaye kufanikiwa kufunga bao la
pili lililowahakikishia ushindi wao katika mchezo huo.
MABAO
Didier Kavumbangu, aliyeandikia bao la kwanza Yanga katika
mchezo huo, aliweza kutikisa nyavu baada ya kutumia udhaifu wa mabeki wa Simba,
ambao walimwacha peke yake wakati aliporuka kichwa kwa kujizungusha mwili na
kumtesa kipa Kaseja.
Shambulizi hilo lililovaa bao lilikuja baada ya kona
iliyochongwa kutoka wingi ya kulia na kiungo, Haruna Niyonzima, ambapo ni
kushoto kwa upande wa Kaseja, ilionekana kama haina madhara, lakini kitendo cha
mabeki wa Simba kumwaacha huru Kavumbagu kiliwagharimu na hatimaye kutikisa bao
hilo lililowainua mashabiki wa timu tangu dakika ya tano ya mchezo.
Kona hiyo iliyokana na shambulizi lililopangwa na Simon
Msuva kwenye wingi ya kulia, ulimsababisha beki Haruna Shamte kuutoa mpira nje.
Wakifungwa bao hilo baada ya tukio la mipira ya adhabu,
jambo hilo lilizidi kuwaonyesha Simba kuwa ni wadhaifu wa mipira ya aina hiyo
baada ya kuruhusu bao jingine katika kipindi cha pili baada ya mpira wa
kurushwa kumkukuta kweupe Hamis Kiiza na kuukwaamisha nyavuni kwa staili ya
aina yake.
Twite alirusha mpira kutoka upande wa kulia, karibu kidogo
na kibendera cha kona, mpira ambao kabla ya kumfikia Kiiza 'Diego', ulionekana
kumbabatiza mchezaji wa Simba kabla ya mfungaji kutumia tena faida ya kujisahau
kwa mabeki wa Wekundu hao wa Msimbazi kuusukuma mpira nyavuni na kuifanya timu
yake kuongoza kwa mabao 2-0, ushindi ambao ulidumu hadi filimbi ya mwisho.
WASHAMBULIAJI
Kama kuna kocha ambaye atajivunia kikosi chake au
washambuliaji wake katika mchezo huo basi ni Brandts wa Yanga, ambao ushindi
wao wa mabao 2-0, shukrani kwa kazi nzuri za Kavumbagu na Kiiza.
Kwa upande wa Simba, Ngassa alipoteza nafasi moja nzuri,
ambapo shuti lake lilipaa pembeni ya goli, huku Felix Sunzu naye akishindwa
kutumia nafasi kadha alizopata baada ya kuingia akitokea benchi.
MABEKI
Ukitazama aina ya mabao ambayo Simba ilifungwa na
kusababisha kupoteza mchezo huo wa jana ilitokana na kukosekana kwa umakini
kwenye safu ya ulinzi, tofauti na wenzao Yanga - ambao ilikuwa imara zaidi
kwenye safu yake ya ulinzi na kuhakikisha inazima mashambulizi yote
yaliyoelezwa kwa goli lao.
Simba wao mabeki wao walitoa nafasi kwa washambuliaji wa
Yanga kuwa huru, jambo ambalo walilitumia kuwaadhibu kwa kuwafunga mabao hayo
mawili.
Kwa upande wa Yanga, safu yake ya ulinzi ilichokuwa ikifanya
ni kuhakikisha mipira yote inayomfikia kipa wao, Barthez ni ile ambayo haina
madhara sana.
MABADILIKO
Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Liewig kwa upande wake alifanya
mabadiliko ya wachezaji watatu, ambapo aliwaigiza Sunzu, Jonas Mkude na
Ramadhan Singano 'Messi' kuchukua nafasi za akina Abdallah Seseme, Amri Kiemba
na Haruna Chanongo, mabadiliko ambayo yalionekana kubadilisha kasi ya mchezo
kwa Simba na kuwapa presha mabeki wa Yanga katika dakika 10 za mwisho.
Messi, alionekana kuwa tishio zaidi kwa mabeki hao wa Yanga
na kumsumbua Luhende mara kadha, licha ya beki huyo wa kushoto kucheza soka la
aina yake katika mechi hiyo ya watani kwa jana.
Lakini, ilionekana kama amechelewa sana kocha Liewig kufanya
mabadiliko hayo, kwasababu licha ya purukushani kadha kwenye goli la Yanga,
mabingwa hao waliweza kuhimili vishindo na kuweza kutimiza ahadi yao ya
kuifunga Simba.
Brandts yeye alifanya mabadiliko ya wachezaji wawili ambapo
aliwatoa Twite na Kiiza na nafasi zao kuingia, Nizar Khalfan na Juma Abdul,
mabadiliko ambayo nusura yazaye bao la tatu baada ya shuti laki la mpira wa
adhabu lililopigwa na Nizar kugonga mwamba kabla ya kumjeruhu Kaseja kichwani
na kumfanya ahitaji huduma ya kidaktari kwa dakika kadha.
Nizar alifyatuka shuti lake nje ya eneo la 18, ambapo shuti
hilo Kaseja aliliguswa kidogo kabla ya kwenda kugonga mwamba na kurudi uwanjani
kupiga kichwani kipa huyo na kupata maumivu.
VITUKO
Kituko kikubwa ambacho kilionekana kuwavutia wengi ni pale
shabiki wa Yanga, aliyekuwa amejipaka masizi na kuvaa nguo zenye rangi ya jezi
za klabu hiyo kwenda kulishika kombe lililokuwa limewekwa pembeni ikisubiriwa
kukabidhiwa kwa mabingwa.
Lakini, kama kituko hicho hakitoshi, baada ya filimbi ya
mwisho na tukio la kugawa medali kumalizika na Yanga wakiwa wamekabidhiwa taji
lao hilo, kundi la mashabiki wa Yanga walionekana wakimbeba juu juu fowadi wa
Simba, Ngassa - huku wakiwa wamemvisha jezi yenye rangi ya kijani na nyano.
Wakati hilo likifanyika, kwenye jukwaa la mashabiki hao wa
Yanga, kulikuwa na bango lililoandikwa 'Ngassa mwana mpotevu karibu nyumbani',
tukio ambalo lilikwenda sambamba na mashabiki hao waliokuwa wamembeba juu juu
mkali huyo wa kimataifa wa Tanzania.
MWAMUZI
Mara kadha kumekuwa na malalamiko kwa waamuzi zinapokuja
kuchezesha mechi kama hizi za watani, lakini kwa refa wa mchezo huo wa jana,
Saanya, haikuwa siku ngumu sana kwake kwani alionekana kumiliki vizuri mchezo
kabla ya kutokea kwa tukio la kujeruhiwa jichoni na kutoka damu wakati
alipokwenda kujaribu kuzuia ugomvi baina ya Kavumbangu na Nassor Masoud
‘Chollo’ na hivyo alianguka na kutibiwa
kwa dakika kadha hadi alipoinuka kuendelea na mchezo kwa sekunde chache na
kupiga filimbi ya mwisho kuhitimisha dakika 90.
VIKOSI
Simba SC: Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Haruna
Shamte, Mussa Mudde, Shomary Kapombe, William Lucian ‘Gallas’, Mrisho Ngassa,
Mwinyi Kazimoto, Abdallah Seseme/Ranmadhani Singano ‘Messi’, Amri Kiemba/Jonas
Mkude na Haruna Chanongo/Felix Sunzu.
Yanga SC, Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite/Juma Abdul,
David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva, Haruna
Niyonzima, Frank Domayo, Didier Kavumbangu na Hamisi Kiiza/Niaar Khalfan.
MATOKEO MENGINE
Wakati pazia la Ligi Kuu Bara likiwa limefungwa rasmi jana,
viwanja kadha vingine vilishuhudia mechi kali kabisa, ambapo JKT Oljoro
walikubali kichapo cha mabao 1-0 kutoka kwa Azam, huku JKT Mgambo wakiinyuka
African Lyon mabao 1-0, Toto Africans
wakiishinda Ruvu Shooting 2-0, JKT Ruvu waliikamua Mtibwa Sugar 1-0 na Tanzania
Prison ilinyukwa 1-0 na Kagera Sugar na Polisi Moro kuichapa Coastal Union 2-0.
No comments:
Post a Comment