VINARA wa Ligi Kuu Bara, Azam leo wamelazimishwa
sare ya mabao 2-2 na Simba katika mechi iliyochezwa kwenye uwanja wa Taifa Dar
es Salaam.
Wakati Azam ikipata matokeo hayo, mabingwa watetezi wa
ligi hiyo, Yanga nao walishindwa kuibuka na ushindi kwenye uwanja wa Mkwakwani
Tanga na kutoka sare ya bila kufungana dhidi ya Mgambo.
Matokeo hayo yanafanya timu hizo kugawana pointi
moja moja humu Azam ikiendelea kukaa kileleni baada ya kufikisha pointi 26,
Yanga ikishika nafasi ya pili kwa kufikisha pointi 24 na Simba ikiwa na pointi
22 katika nafasi yake ya nne.
Kwenye uwanja
wa Taifa Dar es Salaam, mpaka mapumziko timu zilikuwa sare ya bao 1-1, Azam
ikianza kupata bao la kuongoza lililofungwa na John Bocco sekunde ya 58 na Ibrahim Hajib akiisawazishia
Simba katika dakika ya 24.
Kuingia kwa bao hilo kuliichanganya Azam ambapo
waliruhusu mashambulizi mfululizo langoni mwao na kama si uimara wa kipa Aishi
Manula, Simba ingepata mabao mengi.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku kila timu
ikicheza kwa tahadhari na Hajib akaiongezea Simba bao la pili katika dakika ya
68 kwa shuti kali.
Dakika chache baadae Bocco aliisawazishia Azam bao
hilo na kufanya mchezo uzidi kuwa mgumu huku kila upande ukisaka ushindi katika
dakika zilizosalia bila mafanikio.
Kwenye uwanja wa Mkwakwani Tanga, timu zote
zilishambuliana kwa zamu na mpira ulikuwa wenye rafu nyingi kwa wachezaji wa
pande zote.
Katika mechi nyingine Majimaji ikiwa nyumbani Songea
imelala kwa mabao 4-0 kutoka kwa Toto Africans huku Mbeya City ikitoka sare ya
mabao 2-2 na Mtibwa Sugar kwenye uwanja wa Sokoine Mbeya.
Kwenye uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora Kagera
Sugar ilitoka sare ya bao 1-1 na Ndanda huku Stand United ikiambulia kipigo cha
mabao 2-0 kutoka kwa Mwadui.
No comments:
Post a Comment