Licha ya kuondolewa
katika kinyang'anyiro cha kufuzu kwa kombe la dunia Harambee Stars ya
Kenya imepanda nafasi 27 katika orodha ya hivi punde ya Shirikisho la
soka duniani FIFA.
Kenya iliyokuwa imeorodheshwa katika nafasi ya
125 iliwashangaza wengi ilipoilaza Cape Verde bao 1-0 katika mkondo wa
kwanza wa mchujo wa kuwania kombe la dunia.Kufuatia ushindi huo Kenya ilijizolea alama 345 na sasa inaorodheshwa katika nafasi ya 25 barani Afrika na 98 duniani.
Timu hiyo hata hivyo ililazwa 2-0 katika mechi ya marudiano na ikabanduliwa nje ya mchujo huo wa kufuzu kwa mashindanoa hayo.
Kichapo hicho kilifuatia purukushani iliyosababisha timu hiyo kukosa usafiri kwa zaidi ya saa 12 wakiwa katika angatua ya Wilson mjini Nairobi.
Kenya ilifika Cape Verde saa mbili tu kabla ya kuanza kwa mechi hiyo ya marudio na hivyo haikuwa ajabu ilipolazwa 2-0.
Orodha ya mataifa Afrika Mashariki
98 Kenya (imepanda nafasi 27)
-
63 Uganda
-
101 Rwanda
-
112 Burundi
-
132 Tanzania
Kenya inashikilia nafasi ya pili katika mataifa yaliyoimarika nyuma ya Libya iliyopanda nafasi 32 kote duniani.
Katika kanda ya Afrika Mashariki , Uganda ndio inayoongoza ikiwa katika nafasi ya 63 duniani na 13 Barani Afrika.
Kenya (25), Rwanda (27) Burundi 33 na Tanzania 42 zinafuatia.
Barani Afrika Cote de Voire, Algeria, Ghana, Cape Verde na Tunisia ndizo zinazoshikilia nafasi za kwanza tano.
Duniani Ubelgiji Argentina Uhispania Ujerumani Chile Brazil Ureno Colombia England Austria zinashikilia nafasi 10 za kwanza.
No comments:
Post a Comment