KAMATI
ya rufaa ya
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imetupa rufaa ya Dr. Devota John Marwa, juu
ya jina lake kuenguliwa kwenye orodha ya wagombea wa TWFA na kamati ya uchaguzi
wa soka la wanawake.
Akitoa ufafanuzi
wa shauri hilo Mwenyekiti-Kamati ya Rufani za Uchaguzi ya TFF, Julius M. Lugaziya
alisema utaratibu wa kuwasilisha rufani ulikiukwa, na hapa ndipo rufaa hii
inapokwaa kisiki. Chini ya Ibara ya 13 (1) cha Kanuni ya Uchaguzi
(Electoral Code), mgombea ambaye hakuridhika na maamuzi, atawasilisha rufaa
yake ndani ya siku 3 (tatu) tangu uamuzi anaoupinga ulipotolewa.
“Kipengele cha 3
(tatu) cha ibara hiyo kinasema kwamba Mrufani yoyote atakuwa na uhalali endapo
rufaa yake imewasilishwa kwa mujibu wa kanuni hizo. Uamuzi unaolalamikiwa
ulitolewa tarehe 22 Julai 2015, sababu za rufaa ziliandaliwa tarehe 27 Julai na
sababu hizo za rufaa zililipiwa tarehe 28 Julai, 2015. Ni dhahiri kwamba rufaa
ililetwa nje ya muda uliowekwa na kanuni, na kwa hiyo inakosa uhalali kisheria
na kikanuni”, alisema Lugaziya.
Pia alisema japo
katika mwenedo na maamuzi yake Kamati ya Rufani za Uchaguzi haifungwi na
taratibu za kimahakama, suala la muda wa kuwasilisha rufani sio miongoni mwa
mambo ambayo Kamati inaweza kutoyazingatia kwa sababu hiyo, Rufaa hii imetupwa,
lakini kwa sababu tofauti na zile za Kamati ya Uchaguzi.
Lugaziya alisema
Kamati ya Rufani za Uchaguzi inapenda kwa namna ya kipekee kumpongeza mrufani
kwa jitihada alizozionesha kutaka kuitumikia TWFA. Ni matumaini ya Kamati kuwa
hatokata tamaa, na kwamba atakuwa tayari, akitakiwa kufanya hivyo, kupitia
taalum yake, kushirikiana na wenzake katika jitihada za kuendeleza soka la
akina mama lililo na changamoto lukuki.
Mwomba rufani,
Dr. Devota John Marwa, (Mrufani) ni msomi mbobezi katika taaluma ya michezo,
akiwa ni mhadhiri katika kitengo kinachojihusisha na taaluma ya michezo katika
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na aliomba kugombea uenyekiti wa Chama cha Mpira
wa Miguu wa Wanawake(TWFA).
Maombi yake
yalikumbana na pingamizi zilizoletwa na Bi. Chichi Mwidege na Bi. Mwajuma Noty,
ambao kwa pamoja walimwekea pingamizi Mrufani, kwamba hakidhi matakwa ya kanuni
za kugombea nafasi ya Mwenyekiti katika Kanuni za Uchaguzi za TFF Ibara ya 9
(tisa) kipengele cha 3 (tatu), kinachomtaka mgombea awe amejihusisha na uongozi
wa mpira wa miguu kwa muda usiopungua miaka mitano.
Aidha
Ibara ya 28 kipengele cha 3 (tatu), kinamtaka mgombea awe amejihusisha japo
miaka miwili katika shughuli za maendeleo ya mpira wa miguu nchini.
Kamati ya
Uchaguzi iliridhia mapingamizi hayo na kuliondoa jina la mrufani katika orodha
ya wagombea wa nafasi hiyo ya Mwenyekiti.
No comments:
Post a Comment