KOCHA Mfaransa, Patrick Liewig, akizungumzia mikakati yake ya kiufundi baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili kuifundisha timu ya soka ya Stand United ya Shinyanga, kwenye makao makuu ya kampuni ya Acacia jijini Dar es Salaam leo Jumatatu Julai 20, 2015. Mkataba huo ni chini ya udhamini mnono wa kampuni ya Acacia, inayomiliki migodi mitatu ya kuchimba dhahabu ya Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara
Na K-VIS MEDIA
KLABU ya soka ya Stand United ya mjini Shinyanga, imesaini mkataba wa miaka miwili na kocha Mfaransa, Patrick Liewig, ili kuinoa timu hiyo itakayoshiriki ligi kuu soka Tanzania bara msimu huu.
Akizungumza wakati wa kutiliana saini mkataba huo kwenye ofisi za wadhamini wakuu wa timu hiyo, Acacia, jijini Dar es Salaam leo Julai 20, 2015, mwenyekiti wa Stand United, Amani Vincent alisema, baada ya kuangalia vigezo mbalimbali ambavyo klabu hiyo ilihitaji, imeridhika pasina shaka kumuajiri kocha huyo, ili ainoe timu yake kwa misimu miwili.
“Kocha huyu kama mjuavyo anayo sifa ya kuinua vipaji, na sisi tunataka kutengeneza vipaji kutoka chini ili wachezaji hao waweze kuichezea timu yetu”, amesema.Kocha huyo aliwahi kuifundisha Simba ya Dar es Salaam, kwa miezi sita kabla ya mkataba wake kusitishwa.Stand United ambayo inashiriki ligi nkuu ya soka Tanzania bara kwa mara ya pili, hivi karibuni ilipata udhamini mnono kutoka kampuni ya uchimbaji madini, Acacia.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Liewig, amesema, atahakikisha anajenga msingi mzuri timu hiyo kwa kuwa na timu ya kikosi cha wachezaji chipukizi ili iwe na hazina ya wachezaji. “Kinachohitajika ni kuwa na subira, kwani ninataka kujenga timu na kazi hii siyo ya mara moja.”amesema.
Pamoja na mabo mengine, udhamini wa Acacia kwa timu hiyo ni pamoja na malipo ya kocha.
MWENYEKITI wa Stand United ya Shinyanga, Amani Vincent, (wapili kulia), akibadilishana hati za mkataba na Kocha Mfaransa, Patrick Liewig, makao makuu ya kampuni ya Acacia, jijini Dar es Salaam leo Jumatatu Julai 20, 2015. Kulia ni Afisa Habari na Mawasiliano wa Acacia, Frederick Njoka
Liewig, (kushoto), na Amani Vincent, "wakimwaga" wino
Liewig, (kulia), akizungumza na waandishi wa habari
No comments:
Post a Comment