MKE wa Rais, Mama Salma Kikwete leo ameongoza maelfu wa
watu waliojitokeza kumzika aliyekuwa mwanamuziki mahiri wa muziki wa dansi,
Ramadhani Masanja, Banza Stone, katika makaburi ya Sinza.
Msiba huo pia ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa
serikali, wanasiasa pamoja na wadau wengine wa muziki wa hapa nchini.
Mama Kikwete baada ya kuwasili alipokewa na Mbunge wa Jimbo
la Ubungo, John Mnyika, Mkurugenzi wa Baraza la Sanaa la Taifa, Godfrey Mngereza
pamoja na wadau wengine wa siasa na muziki.
Baada ya kupokewa alikwenda moja kwa moja ndani na kuwapa
pole wafiwa ambapo alizungumza na mtoto wa mwanamuziki huyo, Haji Masanja.
Katika mazungumzo hayo gazeti hili lilisikia mama huyo
akimhoji kuhusu shule anayosoma na kidato alichopo, ambapo awali mtoto huyo
wakati akizungumza na gazeti hili alionesha wasiwasi na mustakabali wa
maendeleo ya elimu yake baada ya kifo baba yake.
Awali kabla ya kuwasili kwa Mama Kikwete, watu mbalimbali
walizungumzia kifo hicho cha mwanamuziki huyo ambapo Mngereza kwa upande wake
aliwataka wanajamii kukumbuka ujumbe uliokuwa ukitolewa na mwanamuziki huyo
kwenye nyimbo zake.
Alisema kuwa mwanamuziki Masanja alikuwa akiimba kuhusu
matukio na masuala muhimu katika jamii, ambazo zinaacha mwelekeo wa fikra na
kutoa falsafa ya maendeleo.
Alichukulia mfano wa moja kati ya ujumbe wa mwanamuziki huyo
katika nyimbo zake ambapo kuna wimbo wa Mtaji wa Maskini ni nguvu zake mwenyewe
ambapo ndani yake anawataka watu kufanya kazi kwani kazi ni msingi wa maisha.
"Ule wimbo mimi tangu nimeusikia hadi leo naona kuwa
una ujumbe ambao hauishi mantiki yake na hautaisha kwa kuwa wananchi wanaambiwa
kuwa fanya kazi kwani kazi ni msingi wa maisha na alikuwa akitoa maana halisi
ya sanaa kuwa ni kuelimisha jamii,” alisema Mngereza.
Kwa upande wake Mnyika aliwataka vijana kumchukulia
mwanamuziki huyo kama mfano kwa suala zima la kujituma na kutumia kipaji chake
kwa faida ya maendeleo ya jamii.
Alisema kuwa Banza alikuwa akiimba na alikuwa akiimba
maendeleo pia huku akiwa ni kijana ambaye ameibukia kutokea Sinza ambapo kuna
vijana wengi na wenye kuweza kufanikiwa kama mwanamuziki huyo alivyofanya.
Kwa upande wake mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Sinza A,
Kasim Said Kabuluu alisema kuwa mwanamuziki huyo alikuwa ni kama nguzo ya
serikali yake katika kuzungumzia masuala mbalimbali na vijana wenzake.
No comments:
Post a Comment