Uongozi
wa klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam umekumbushwa kurejea kwa
wazee wa klabu hiyo ili kupata baraka za kuiongoza klabu hiyo ambayo
kwasasa inaonekana imeanza kunyemelewa mgawanyiko mkubwa wa wanachama
wake.
Akiongea
na mtandao wa Rockersports nyota wa zamani wa klabu hiyo ambaye pia
aliwahi kuwa katibu mkuu na mdhamini katika vipindi tofauti Hamisi Ally
Kilomoni ameonekana kushangazwa na uongozi ulioko madarakani kwa sasa
chini ya Rais Evance Aveva, kuwa umewasahau wazee wa klabu hiyo ambao
wamepata shida na klabu hiyo katika vipindi mbalimbali vya uongozi wa
klabu hiyo.
Kilomoni
amesema huko nyuma haikuwahi kutokea kwa wanachama wa klabu hiyo
kufukuzana uanachama jambo ambalo amesema endapo Aveva atashindwa
kuwaita wazee wa klabu hiyo kupata muafaka wa wanachama waliotimuliwa
basi huenda mambo yakaenda mrama katika uongozi wake.
Aidha
amekanusha kulikumbatia kundi lililojitokeza hivi sasa maarufu kama
'UKAWA' ambalo linaonekana kuwa na joto la upinzani ndani ya klabu hiyo
ambalo sehemu kubwa ya wanachama wake walitumuliwa na mkutano mkuu wa
wanachama wa klabu hiyo kutokana na kuelekea mahakamani kupinga maamuzi
ya kuenguliwa katika kinyang'anyiro cha uchaguzi kwa Michael Wambura
aliyekuwa mnpinzani wa Aveva.
Mzee
Kilomoni ambaye aliondolewa katika nafasi ya udhamini wa klabu hiyo
yeye na mzee Abdul Wahabu amesema pamoja na kwamba klabu hiyo inaongozwa
na vijana ambao wanataka kuiongoza kisasa lakini bado kuna watu walio
hai ambao wamepata tabu katika kuijenga klabu hiyo tangu zama za jina la
Sunderland katika miaka ya 1960's tena kwa kuchangia fedha zao za
mifukoni.
No comments:
Post a Comment