Wanariadha wa Kenya wameapa kupinga mpango wa serikali wa kuwalazimisha kulipa kodi kutokana na mapato yao.
Siku ya Jumanne, Shirika la utozaji ushuru
nchini Kenya KRA lilitangaza kuwa mapato yote watakayoshinda wanariadha,
ikiwa ni pamoja na wachezaji wa soka nje na ndani ya nchi ni sharti
yatozwe ushuru kuanzia mwezi huu.
Lakini wanamichezo hao ambao
huchangia kiasi kikubwa cha mapato yao katika uchumi wa taifa,
wametishia kususia mashindano yote ya kimataifa ikiwa serikali
itaendelea na mpango huo wa kuwatoza ushuru.
Wanariadha hao wamesema fedha wanazopata sio
nyingi kwani huwa hawashindi hela kila mwezi na huenda ikawachukua zaidi
ya miaka mitano kujiinua tena ikiwa serikali itawatoza ushuru.
Wakiongea mjini Eldoret, Magharibi mwa Kenya
wanariadha hao, wakiongozwa na mbunge wa Cherangani ambaye pia ni bingwa
wa zamani wa mbio za Boston Marathon Wesley Korir,wanadai kuwa KRA
haina mfumo dhabiti wa kubaini kiasi cha fedha walizoshinda wanariadha,
kwa sababu shirika hilo halijaorodhesha mbio walizo shiriki na kiasi cha
fedha walizoshinda.
Mwaka wa 2012, wanariadha kadhaa akiwemo
mshikilizi wa rekodi ya dunia wa mbio za mita mia nane kwa upande wa
wanaume David Rudisha, bingwa mara mbili wa dunia wa mbio za Marathon
Abel Kirui, walikabithiwa nyaraka na KRA kuwataka kulipa malimbikizi ya
kodi inayokisiwa kuwa mamilioni ya madola.
No comments:
Post a Comment