Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Wednesday, November 6, 2013

TANZANITE YAWAAHIDI WATANZANIA USHINDI DHIDI YA MSUMBIJI


MKURUGENZI Msaidizi wa Maendeleo ya Michezo wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Juliana Yassoda ameikabidhia timu ya taifa ya wanawake chini ya miaka 20 Tanzanite bendera kwa ajili ya kwenda Msumbiji kwenye mechi ya  marudiano kuwania kufuzu Kombe la dunia mwakani.

Timu hiyo ikiwa na wachezaji 16 tayari iliondoka jana mchana  huku wachezaji wengine wanne wakibaki kwa ajili ya mitihani, lakini mara baada ya kumaliza mitihani hiyo  Ijumaa wataenda kuungana na wenzao.
Yassoda alikabidhi bendera hiyo jana kwenye Ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF)  kwa nahodha wa timu hiyo Fatma Issa.

Akizungumza mara baada ya kukabidhi bendera hiyo Yassoda alihimiza timu hiyo kwenda kuwa mabalozi wazuri kwa kujitahidi ili kurudi na ushindi.
Alisema  timu hiyo  inaweza kufika mbali ikiwa wafadhaili mbalimbali watajitokeza katika kuiunga mkono.

 “Ni muhimu watu wajue kuwa timu yetu ina uwezo mkubwa kutangaza biashara zao ikiwa wafadhili watajitokeza katika kuwaunga mkono, tuwasaidie ili wapate hamasa ya kufanya vizuri zaidi,”alisema Yassoda.

Alisema wachezaji hao wanahitaji kuendelezwa kielimu na kinidhamu kwa lengo la kufanya vizuri  wakati ujao.
Kwa upande wake, Kocha wa timu hiyo Rogasian Kaijage alisema vijana wako tayari kupigana  kwani wameandaliwa vizuri.

Alisema vijana hao sio tu wameandaliwa kwa ajili ya michezo hii  bali wanahitajika kuandaliwa kwa ajili ya kuwa wachezaji wazuri wakati ujao, ili kuisaidia timu ya Taifa ya Twiga Stars kwenye mashindano ya kidunia.

Naye Nahodha wa timu hiyo Fatma Issa amewaahidi watanzania kuwa watafanya vizuri hivyo kuwaomba kuwasaidia ufadhili kama ilivyo kwa timu ya Taifa ya wanaume ili kupata hamasa.
Mchezo wa marudiano na Msumbiji wa kutafuta kufuzu kombe la dunia  utachezwa Novemba 9. Katika mchezo wa awali,  Tanzanite iliwafunga Msumbiji mabao 10-0.

Kikosi cha Tanzanite kinaundwa na wachezaji Celina Julias, Nadiat Abbas hawa ni makipa, Stumai Abdallah, Maimuna Said, Fatuma Issa, Anastazia Anthony,  Dionisia Daniel, Vumilia Maarifa, Amina Ali, Neema Paul, Shelder Boniface na Theresia Yona.

Wengine ni Tatu Iddi, Happyness Lazoni, Hamisa Athuman Amina Hebron, Rehema Abdul, Sabai Hashimu, Amina Ramadhan na Latifa Ahmad.

Fainali za Dunia za U 20 kwa wanawake zitafanyika mwakani nchini Canada. Iwapo Tanzania itaitoa Msumbiji katika raundi hii, raundi inayofuata itacheza na mshindi kati ya Botswana na Zimbabwe na  ikifanikiwa kupita Tanzania itashiriki kwa mara ya kwanza michuano hiyo ya Kombe la Dunia kwa wasichana.


No comments:

Post a Comment