KATIKA hali ya kutaka kuondoa ‘uteja’ wa kufungwa na Mtibwa mara mbili kwenye msimu wa Ligi Kuu uliopita, Kocha Mkuu wa timu ya Simba, Abdallah Kibadeni, amesema lazima katika mechi ijayo ahakikishe wanalipiza kisasi.
Simba watakuwa wenyeji wa Mtibwa Sugar katika mchezo utakaofanyika katika Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam Septemba 14, mwaka huu.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, kocha huyo alisema kuwa silaha zote wanazozitegemea Mtibwa anazifahamu na kwamba atahakikisha anatumia zilaha zake kila mbinu kuwaangamiza.
“Mtibwa Sugar si lolote kwetu, kwa sababu nafahamu mbinu zao na pia wachezaji wao tegemeo, hivyo lazima katika mechi ijayo tuibuke na ushindi mnono pamoja na kuwapa raha mashabiki," alisema Kibadeni
Aidha kocha huyo aliwataka mashabiki na wapenzi wa Simba kuwa wavumilivu, ili kutoa nafasi kwake kuleta mabadiliko katika timu hiyo msimu huu na kurudisha hadhi yao kama ilivyokuwa zamani.
Simba inaingia uwanjani kupambana na Mtibwa Sugar, ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa jumla ya mabao 3-0, baada ya mechi ya kwanza wakata miwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 mjini Morogoro na mchezo wa pili waliibuka na ushindi wa bao 1-0 jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment