MAJOGOO wa Merseyside, klabu ya Liverpool, haina kikubwa cha
kujivunia katika usajili wa majira haya, zaidi ya kujivunia kunasa saini ya
mlinda mlango wa Sunderland, Simon Mignolet. Liverpool 'The Reds,' licha ya
kuingiza nyota kama Kolo Toure, Iago Aspas na Luis Albertom, lakini ina kila
sababu ya kujivunia ujio wa Mignolet, aliyenaswa kwa ada ya pauni milioni 9.
Haimaanishi ndiye mchezaji ghali ama wa bei chee katika
lugha ya kifedha, la hasha, sema umahiri wake langoni, unamfanya awe kipa
sahihi kwa Majogoo hao, walioanza kupoteza matumaini ya kurejesha umaarufu wao,
ikiwa ni msimu wa nane bila chochote kikubwa.
Liverpool, tangu watwae ubingwa wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA)
2005, kwa kudra za kipa Jerzy Dudek, aliyezima ndoto za AC Milan, waliokuwa na
uhakika wa kutwaa ubingwa huo kwa kuwa mbele kwa mabao 3-0, kipindi cha kwanza,
lakini hadi dakika 120, ubao wa matokeo ulikuwa ukisoma 3-3, hivyo kulazimika
kuamuliwa kwa mikwaju. Heshima ya Liverpool, iliokolewa na Dudek kwa kupangua
mkwaju wa Andrey Shevichenko, wakatwaa ubingwa wa tano, ikiwa ni rekodi ya
kipekee kwa England. Hakuna timu iliyofikia idadi hiyo mpaka sasa.
Kumalizika kwa sherehe za 'ubingwa wa maajabu,' mkombozi
Dudek, aliamua kutafuta changamoto mpya na kuhamia Real Madrid na nafasi yake
kurithiwa na Jose Manuel Paez 'Pepe' Reina, aliyetokea Villarreal ya Hispania.
Reina alitabiriwa 'angevaa miwani' ya Dudek na kuendeleza mafanikio
aliyoyakuta. Gafla haikuwa hivyo, kinyume chake aliibuka kuwa mwanzo wa mikosi
na laana iliyoiandama Liver, ambayo leo hii hadhi yake haithaminiki tena.
Kenny 'King' Dalglish, Roy Hogson, na sasa Brendan Rogers,
wamepewa jukumu la kuhakikisha wanarudisha heshima hiyo kama alivyofanya Rafael
Benitez 2005, lakini hata matumaini ya kucheza Ligi ya Ulaya (Europa), yanazidi
kupungua msimu hadi msimu.
Turudi kwenye mada ya kipa Reina. Pamoja na kuaminishwa kuwa
kipa namba moja, katika miaka nane aliyokaa Anfield, uzoefu wake na timu ya
taifa ya Hispania, na kwenye michuano mikubwa kama Uefa, ikiwemo kucheza
fainali 2007, lakini mechi 400 alizoidakia Liverpool, hazikuwa na maana yoyote,
kwani ameshindwa kuwapa taji la thamani kama makipa waliomtangulia.
Ujio wa Mbelgiji Mignolet (25), ambaye mwaka jana
alichaguliwa kuwa mchezaji bora kwenye tuzo za Umoja wa Waandishi wa Habari
London Kaskazini Mashariki, ana kila dalili za kurejesha kile Tom Hicks na
George Gillett na sasa John W. Henry (wamiliki) walichohitaji miaka
yote-kuisuka upya Liver irudi kuwa timu ya upinzani EPL .
Katika tuzo hizo, Mignolet aliwabwaga kipa Tim Krul na
mshambuliaji Hatem Ben Arfa (wote wa Newcastle), walioingia tatu bora. Lakini
pia alitajwa kuwa kipa wa pili kwa kupangua mashuti mengi langoni msimu wa
2012/13, nyuma ya kipa wa West Ham, Jussi Jaaskelainen, huku akimaliza msimu
akiwa nafasi ya nne kwa ubora wa makipa, kwa mujibu wa tovuti ya EA Sport.
Mafanikio, uwezo na umahiri wake langoni, ulimpa kiburi
aliyekuwa Kocha wa Sunderland, Martin O’neill, aliyekaririwa akisema 'kubaki
kwa Sunderland Ligi Kuu ilihitaji nguvu ya mchezaji mmoja tu na Mignolet ndiye
anaweza kufanya hivyo,' na kweli ilifanikiwa kubaki, ingawa ilimaliza msimu
ikiwa chini ya 'mtukutu' Paolo Di Canio.
Ahadi ya kwanza ya mmiliki Henry, ilikuwa ni kuhakikisha
Liverpool, inarejesha heshima, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha hali ya uchumi.
Kwa mujibu wa tovuti ya klabu hiyo ‘Thisi is Anfield’,
iliripoti kuwa msimu uliopita ilishuka mpaka nafasi ya 21 kutoka 18, katika
masuala ya kuvuna mkwanja. Sababu iliyotajwa ni kukosekana kwenye mashindano
makubwa kama Uefa na nne bora za Ligi Kuu. Kuporomoka huko, kumemfanya mmiliki,
Henry kuwaandikia wadau wa timu hiyo barua ya wazi kuhusu mradi alionao -
kuijenga upya Liverpool ikiwa ni kumpatia uhuru kocha kwenye usajili.
Na kweli Rogers, pamoja na kuwepo pengo la kiungo mkabaji na
mshambuliaji wa pili (No.10), kwa upande wa pili, alitumia jicho la tatu
kutafuta kipa mwenye kutembelea kivuli cha Dudek, aliyeipa mafanikio, kinyume
na Reina aliyeonekana kuwa mchawi wa mataji Anfield. Swali ni Je, ataweza
kufukia laana za Reina na kufufua mizimu ya Dudek?
Ujio wa Mignolet, unatajwa kama sababu ya Reina kuhamia
Napoli kwa mkopo, pengine alitambua kiwango chake kilikuwa bora mbele ya kina Alexander Doni, Scott Carson,
Brad Jones na Diego Cavalieri, lakini si mbele ya Mbelgiji huyo aliyesimama
langoni mechi zote za Ligi kuu msimu ulipoita.
Msimu uliopita, Reina aliongoza orodha ya makipa waliofanya
madudu 'blunders,' licha ya kucheza mechi chache (31), makosa sita ya kizembe
na kuifungisha timu, pamoja na kufungwa mabao manne rahisi, jumla mabao 10
yalimfanya kuongoza orodha ya makipa 'majuha' wakati Mignolet alifanya makosa
mawili na kufungisha mawili, katika mechi zote (38) za Ligi Kuu na michuano
mingine.
Takwimu zao 2012; Mignolet aliokoa mashuti 149, Reina 73,
wakati uwezo wa kuipa ushindi timu Mignolet 96% Reina 89.
Plani ya kocha Rogers ya kuomba kupewa majukumu ya kuijenga
na kujimwaya mwaya sokoni kumsajili amtakaye, ujio wa kipa bora London, kuna
uwezekano akaibuka mchezaji bora wa Merseyside muda mfupi.
Makala hii imeandaliwa na Nicodemus Sinolest kwa msaada wa
mitandao.
No comments:
Post a Comment