BEKI mpya wa Simba kutoka nchini Burundi, Kaze Gilberty, ametamba
ujio wake ndani ya klabu hiyo utamaliza tatizo sugu la ulinzi ndani ya timu
hiyo.
Kaze, aliyewasili nchini juzi na kusaini mkataba wa miaka
miwili na Simba jana, aliwataka wanachama na mashabiki wa klabu ya Simba kumpa
muda kwanza ili aweze kusoma mazingira pamoja na wapinzani wao kabla ya kuanza
kushusha nondo katika timu yao.
Akizungumza na LENZI YA MICHEZO, muda mfupi baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili, Kaze alisema ametua Tanzania
kwa kazi moja tu, nayo kuhakikisha anaimarisha ukuta wa timu hiyo ili
kuiwezesha kufanya vizuri katika michezo yake.
Alisema binafsi ni mchezaji mzuri na ndiyo maana Simba walimfuata
na kumsajili, hata hivyo ili aweze kuwajibika na kutoa mchango unaohitajika
ndani ya timu, ni lazima apate ushirikiano kutoka kwa wachezaji wenzake.
“Uongozi, wanachama na mashabiki wa Simba wanatakiwa kuwa
wavumilivu na kunipa muda wa kusoma mazingira ya soka ya hapa pamoja na kuelewa
aina ya ufundishaji wa kocha ili nizoee kombinesheni ya timu, nina hakika
nitawafanyia mambo makubwa,” alisema.
Alisema anaomba apewe nafasi ya kucheza mechi dhidi ya
Kombaini ya Polisi, itakayofanyika leo katika Uwanja wa Taifa, ili aweze
kuwasoma wenzake pamoja na kuanza kuzoea mazingira ya Tanzania.
Kaze alisema hana hofu na washambuliaji wa timu pinzani,
kwani uzoefu na mbinu za kibeki alizonazo ana hakika hawataweza kufua dafu
mbele yake, akiwemo raia mwenzake kutoka Burundi anayekipiga na Yanga, Didier
Kavumbagu.
“Kavumbagu namfahamu sana, tulishawahi kucheza timu moja ya
Taifa, pia katika Ligi tulishaonana sana, kwa hiyo kama huyo ndiyo mmoja kati
ya washambuliaji hatari hapa nchini, basi hawataniumiza kichwa.”
No comments:
Post a Comment