SWALI kubwa wakati taarifa za Neymar kusajili
Barcelona zilipotangazwa rasmi, lilikuwa ni vipi Mbrazil huyo atacheza sambamba
na Lionel Messi pale Camp Nou.
Wachambuzi wengi wa soka akiwemo gwiji wa Barcelona,
Johan Cruyff walianza kuishauri Barca kumuuza Messi, kwa sababu walikuwa
wakiamini kwamba wawili hao hawawezi kucheza pamoja.
Kuna ambao walisema kwamba, Neymar ameenda
kujimaliza pale Barcelona na kufuata nyayo za kina Zlatan Ibrahimovic, Alexis
Sanchez na wengine kibao ambao wameshindwa kuvuma Camp Nou.
Baada ya maneno mengi kuhusu namna wawili hao
watakavyocheza pale Barcelona, juzi usiku mwanga ulianza kuonekana jinsi wawili
hao watakavyotumika kwenye kikosi kimoja Barca.
Barcelona walionyesha soka safi Ijumaa usiku, katika
mechi ya Kombe Joan Gamper, walipoibuka na ushindi wa mabao 8-0 dhidi ya
Santos, kwenye mechi ya kwanza ya Neymar mbele ya mashabiki wa Santos.
Mechi hiyo ilikuwa ni sehemu ya makubaliano kati ya
timu hizo mbili katika mauzo ya Neymar, kwenye mechi hiyo Mbrazil huyo alicheza
kipindi cha pili tu na alifanikiwa kuonyesha uwezo wake mbele ya mashabiki
Barca.
Moja ya vitu vilivyozungumzwa sana kabla ya mechi
hiyo, ni jinsi gani kocha mpya wa Barca, Tata Martino atatengeneza kombinesheni
ya Neymar na Messi na kwa dakika chache za kipindi cha pili watu walifanikiwa
kuwaona wote wawili wakiwa uwanjani kwa wakati mmoja.
Hatahivyo, pamoja na kwamba bado hawajarudi kwenye
fomu kutokana na kuwa wametoka mapumzikoni, wapenzi wa soka walifanikiwa kuona
mpango wa Martino kwa wawili hao na vipi watafiti kwenye mfumo wake.
Baada ya mechi hiyo, ilionekana wazi kwamba, Martino
hana mpango wa kubadilisha mfumo uliokuwa ukitumiwa na makocha waliopita kabla
yake, Barca walitumia mfumo wao wa siku zote wa 4-3-3.
Messi alicheza nafasi yake ya siku zote - namba tisa
wa uongo (false nine) na kuongoza mashambulizi na alihusika sana kwenye
kuanzisha ‘move’ za Barca kipindi cha kwanza cha pambano hilo.
Winga wa Kihispaniola, Pedro Rodriguez, alikuwa
akishambulia akitokea kulia na staa wa Chile, Alexis Sanchez akiingia katikati
kutokea kushoto, Messi alikuwa akishuka chini zaidi kuchukua mipira na
kuwachezesha wawili hao waliokuwa pembeni.
Katika mechi hiyo, Barca walirudi kwenye staili yao
ya kucheza na kukabia juu, staili ambayo msimu uliopita haikutumika. Japokuwa
ni mapema sana kusema walifanya vizuri na Santos pia walikuwa wapinzani dhaifu,
lakini staili hii ya kukabia juu ni jambo muhimu sana ambalo lilionekana kwenye
mechi hiyo.
Pale Neymar alipoingia kuchukua nafasi ya Pedro
katika kipindi cha pili, alienda kucheza upande wa kushoto na Sanchez alihamia
kulia katika wale wachezaji watatu wa mbele wa Barca, huku Messi akicheza kati
kati yao kama kawaida.
Staa huyo wa zamani wa Santos hakuwa kwenye kiwango
chake bora juzi, lakini kuna wakati alifanya mambo makubwa na kuthibitisha kile
atakachokifanya kwenye klabu yake mpya.
Alipiga chenga za baiskeli na visigino kwenye mechi
hiyo iliyokuwa ya upande mmoja, pamoja na kwamba mechi hiyo ilikuwa rahisi kwa
Barca cha muhimu ilikuwa namna Neymar alivyotumika. Pande lake lililozaa bao la
pili la Cesc Fabregas, ulikuwa uthibitisho tosha juu ya ubora wake.
Kitu ambacho Neymar ataongeza Barcelona ni soka la
moja kwa moja, kama ambavyo Pedro amekuwa akifanya miaka ya nyuma. Anaweza
kuendana na pasi fupi na za haraka za Barca, lakini pia ni mpigaji mzuri wa
pasi za mwisho na mashuti makali pale watakapokutana na timu ngumu.
Juzi, kulikuwa na dalili za kwamba alitumia nguvu
nyingi kujaribu kufanya mambo makubwa uwanjani na kujiweka kwenye mazingira
magumu. Lakini akizoea mazingira atakuwa mzuri zaidi na atajua wakati gani
afanye nini.
Inawezekana watu hawakuwaona Messi na Neymar kwa
muda mrefu kwenye mechi hiyo dhidi ya Santos, lakini cha muhimu ni kwamba,
imejulikana watatumikaje msimu ujao. Mtihani mkubwa kwao sasa ni jinsi gani
watatengeneza kombinesheni yao.
Hivyo kutokana na tulichokiona juzi, inaonyesha
kwamba kwenye mfumo wa 4-3-3, Messi atakuwa kati kati na Neymar atashambulia
kutokea kushoto, kazi sasa imebaki kwa mabeki kuja na mbinu za kuwazuia, maana
wasipofanya hivyo watauliwa.
No comments:
Post a Comment