DIRISHA la usajili linapofunguliwa, siku zote
huambatana na uvumi wa hali ya juu, mara huyu anaenda huku, yule anaenda kule,
ilimradi fujo tu.
Vyombo vya habari vya Uingereza vimejikita kwenye
kuanzisha uvumi kwa ajili ya mashabiki wa soka ambao siku zote huwa wanatamani
kuona habari ambazo zinawahusisha wachezaji wenye majina makubwa duniani na
klabu zao.
Mashabiki wa Manchester United ndio wamekuwa
wakilengwa kwenye dirisha hili la usajili la kiangazi. Usajili umefunguliwa kwa
mwezi mmoja sasa na hakuna mchezaji mwenye jina kubwa hata mmoja aliyetua
kwenye klabu hiyo.
Kocha mpya, David Moyes amejikuta akipata wakati
mgumu sana kufanya usajili mkubwa kwenye kibarua chake kipya. Wachezaji mastaa
wote alioonyesha nia ya kuwasajili, wamekuwa wagumu kukubali kutua Old
Trafford.
Pamoja na hayo, vyombo vya habari vya Uingereza,
vimeendelea kuihusisha timu hiyo na wachezaji wakubwa, safari hii gazeti la
Daily Star, limeibua upya uvumi wa Cristiano Ronaldo kurudi Old Trafford.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, Rais wa Real Madrid,
Florentino Perez amekuwa kwenye mazungumzo na Man United juu ya uwezekano wa
kumrudisha Ronaldo, Old Trafford.
Gazeti hilo limedai kwamba, sababu kubwa ya kuibuka
kwa sakata hilo ni kitendo cha Real Madrid kuelekeza nguvu zao nyingi kwenye
mbio za kumsajili winga wa Tottenham Hotspur, Gareth Bale kwa ajili ya kuja
kuchukua nafasi ya Ronaldo.
Kama uvumi huo hautoshi kuwafanya mashabiki wa Red
Devils kudata kwa furaha, gazeti lingine la Uingereza la Daily Mail,
limeihusisha klabu hiyo ya Old Trafford na staa mwingine kwenye Ulimwengu wa
soka.
Gwiji wa Man United, Peter Schmeichel aliliambia
gazeti la Sweden la Expressen, kwamba straika wa Paris Saint-Germain, Zlatan
Ibrahimovic utakuwa bonge la usajili kwa kocha mpya wa timu hiyo, Moyes.
“Unaweza kujiuliza kwa nini bado Zlatan
(Ibrahimovic) hajawahi kucheza England, lakini ningependa kumuona akichezea
Manchester United, sijui ni shabiki wa timu gani, lakini naamini alizaliwa
kuichezea Manchester United na atatisha kwenye timu hiyo,” alisema Schmeichel.
Watu wanashindwa kujua mara moja iwapo Schmeichel
anaongeza mafuta ya taa kwenye moto au kuna kitu cha ziada anajua kuhusu
mchezaji huyu na Man United.
Ibrahimovic amewahi kuhusishwa na kujiunga na Man
United miaka ya nyuma, lakini uvumi wake haukushika kasi sana.
La msingi kulitambua hapa ni kwamba, Moyes ananafasi
ndogo sana ya kumnasa mmoja wapo kati ya Ronaldo na Ibrahimovic, achilia mbali
wote wawili.
Lakini tukiachana na ukweli huo, hebu tujiulize
swali la kizushi tu, ambalo linaweza kuwa mjadala mkubwa sana vijiweni, je,
Ibra na Ronaldo wanaweza kucheza timu moja?
Jibu la kwanza kwenye swali hili, linaweza kuwa
kujiuliza iwapo tabia, ubinafsi wa kila mmoja utaweza kuwaruhusu kucheza
pamoja?
Wote wawili wanapenda kucheza kwenye timu ambazo wao
wanachukuliwa kama wachezaji muhimu zaidi. Lakini kutokana na ubora wa kila
mmoja, hilo limekuwa likifanyika, kila wanapoenda wao ndio huwa muhimu ndani ya
vikosi vyao.
Kuna msemo wa Kiingereza usemao; ‘The world cannot
revolve around two suns’ (Dunia haiwezi kuzunguka majua mawili), hivyo timu
haiwezi kufanya vizuri kama itakuwa na mastaa wawili ndani yake.
Kama Moyes alikuwa anajaribu kuwashawishi wote
wawili kutua Manchester, ni wazi kabisa atakuwa anafanya hivyo kutokana na njaa
ya ushindi waliyonayo wote wawili.
Lakini ni ngumu kuamini iwapo wawili hao, wataweza
kucheza pamoja bila kugombana uwanjani mara kwa mara.
Ubora wa wawili hao hauna ubishi, lakini swali ni
je, wanaweza kucheza kwenye kikosi kimoja?
Kati ya wawili hao, Ibrahimovic atahitajika kucheza
kati kati zaidi. Wote ni hatari kwenye mifumo ya timu zao.
Hivyo Ronaldo atapelekwa pembeni, sana sana
atachezeshwa upande wa kushoto.
Lakini ukiangalia mbali zaidi, utagundua kwamba ni
ngumu kwa Ronaldo kuridhika kucheza pembeni muda wote, kuna wakati atataka
kuingia kati kati na kucheza kama mshambuliaji, hapo kazi ndiyo itaanza.
Novemba 2012, Wakala wa Ibrahimovic, Mino Raiola
alinukuliwa na mtandao wa Goal.com akisema kwamba, anaamini mteja wake na
Ronaldo wanaweza kufanya makubwa sana PSG, kwa sababu wachezaji wazuri siku
zote hawapati tabu kucheza pamoja.
Maneno yake kwamba wachezaji bora hawawezi kupata
tabu kucheza pamoja, yanaweza kuwa jibu la makala haya.
Kuna sababu nyingi ambazo zinathibitisha kwamba,
Ibrahimovic na Ronaldo hawawezi kucheza pamoja, lakini kuna sababu moja tu
ambayo inaonyesha kwamba wawili hao wanaweza kufanya makubwa pamoja.
Sababu hiyo moja ambayo inaunga mkono kombinesheni
ya Ibra na Ronaldo ni kwa sababu wote wawili ni bora na wachezaji bora siku
zote hupata njia ya kuipa timu yao ushindi.
Baada ya kujiuliza swali hili la kizushi, tusubiri
kuona iwapo Ibra na Ronaldo watatua Man United na kama wataweza kucheza pamoja,
au ndiyo mmoja atafulia na kumuacha mwingine ang’are.
No comments:
Post a Comment