GARETH Bale alipokea mpira akiwa upande wa kulia wa uwanja,
akauhamishia kwenye guu lake la kushoto, akaingia nao ndani na kuachia shuti
kali la umbali wa yadi 25, lililomshinda kipa wa Sunderland, Simon Mignolet.
Hilo ndilo bao la mwisho la Bale msimu uliopita, ambalo
liliwapa matumaini ya muda ya kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Lakini ushindi wa bao 1-0 walioupata Arsenal dhidi ya
Newcastle United kwenye uwanja wa St James' Park, ulikatisha ndoto na furaha
pale White Hart Lane.
Bao hilo lilikuwa limepunguza presha ya kumbakiza Bale,
White Hart Lane, kwa msimu mwingine kwa sababu lingeweza kuwapeleka ligi ya
mabingwa, lakini ushindi wa Arsenal uliwabakiza nafasi ya nne, na Spurs
wakarudi tena kwenye Europa League. Mafanikio ya Bale baada ya mechi hiyo
yalikosa mashiko.
“Kila la kheri Hispania, Gareth (Bale),” mmoja wa mashabiki
alisikika akisema wakati wachezaji wakiingia kwenye vyumba vya kubadilishia
nguo, tayari walihisi hili linakuja.
Hakuna ambaye anaweza kujua kama kumaliza nafasi ya nne
kungembakiza Bale kwa msimu mwingine na kumshawishi kuongeza mwaka mmoja zaidi
katika ile sita aliyokaa White Hart Lane.
Bale alifurahia sana kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa
2010-11, na kiwango chake dhidi ya timu za Milan kilimtambulisha kimataifa na kiwango
chake huko ndicho kilianza kuzivuta klabu za Real Madrid na Inter Milan. Je,
Bale angejawa na hisia za kipekee, kushuhudia usiku wa Ligi ya Mabingwa kwenye
uwanja wa White Hart Lane tena?
Bahati mbaya kwa Spurs, Madrid ndio wanamtaka Bale na wako tayari
kutoa zaidi ya pauni milioni 80, kwa ajili yake, kwa hiyo hata kama Spurs
wangemaliza katika nafasi ya nne kumbakiza Bale, bado ingekuwa kazi sana, kwa
sababu kama kucheza Ligi ya Mabingwa angeenda Celtic.
Lakini kilichopo hapa, Bale (24) anataka zaidi. Anataka
kuona raha ya kucheza klabu kubwa, ambayo inaweza kuchuana kuwania mataji
makubwa na kupata mafanikio zaidi ambayo Spurs hawawezi kumpa, hivyo ndoto zake
zote ziko Santiago Bernabeu.
Aliizungumzia vizuri klabu hiyo kabla ya kukutana nao kwenye
Ligi ya Mabingwa Ulaya, katika uwanja wa Bernabeu mwaka 2011, msimu ambao Spurs
walishiriki michuano hiyo.
Je, Tottenham watambakiza? Hakuna ubishi kwamba wangependa
kufanya hivyo na wako radhi kufanya lolote. Andre Villas-Boas alimpa Bale
majukumu ya kucheza huru msimu uliopita, akicheza kama namba 10 na uhusiano
kati ya AVB na Bale ni mkubwa. Wamekuwa marafiki wa karibu katika miezi 12
iliyopita.
Halafu kuna huyu Mwenyekiti, Daniel Levy, ambaye ni ngumu
kusema kama yuko karibu na Bale. Amekataa kusikiliza ofa yoyote ya Bale,
japokuwa anaweza kujikuta akilia siku za usoni. Kitendo cha kukataa kumuuza
Luka Modric kwa dau la pauni milioni 40 misimu miwili iliyopita, inaonyesha
jinsi gani anamaanisha anachokisema.
Aliwahi kuwaachia kwa mbinde, Dimitar Berbatov na Michael
Carrick kwenda Manchester United na Modric kwenda Real Madrid.
Hapa kinachoangaliwa ni fedha na kufikia dau analolitaka
Levy, kuliko maombi ya mchezaji kuhama na kwenda kwenye ushindani zaidi.
Alimlipia Bale pauni milioni 5 kutoka Southampton mwaka
2007, lakini ni wazi sasa hivi Bale amekuwa kuliko klabu na ni wakati wake
kuondoka.
Kuna sababu tatu ambazo zinamuondoa Spurs, Bale aliyefunga
mabao 21 kwenye Ligi msimu uliopita.
Kucheza Ligi ya
Mabingwa Ulaya
Linapokuja suala la Ligi ya Mabingwa Ulaya, Bale anauamuzi
rahisi sana, kubaki Tottenham na kucheza Europa League na kusubiri msimu
mwingine kusaka tiketi ya kushiriki michuano hiyo, au anaweza kujiunga na klabu
ambayo imeshinda mara tisa michuano hiyo na inasaka taji la 10. Akiwa Real
Madrid, itakuwa rahisi kwake kushiriki. Wakati huu ambao kiwango chake kiko
juu, Bale anatakiwa kwenda Santiago Bernabeu na kuchezea klabu ambayo imefika
nusu fainali tatu za ligi ya mabingwa katika misimu mitatu iliyopita. Badala ya
kubaki kwenye timu ambayo pamoja na kufunga mabao mengi, imeshindwa kumaliza
katika nafasi nne za juu England, anatakiwa kwenda Madrid na kuungana na Carlo
Ancelotti, aliyeshinda taji hilo mara mbili.
Kukumbukwa milele
Akiwa kama staa wa Tottenham, Bale ameingia kwenye orodha ya
mastaa wa Ligi Kuu England. Chelsea kuna Eden Hazard, Manchester United kuna
Robin van Persie na Liverpool kuna Luis Suarez. Haya ni majina yanayoweza
kuingia kwenye kikosi cha kwanza cha dunia, lakini je, watakumbukwa baada ya
miaka 10?
Labda Van Persie; kutokana na kiwango chake kilichoipa ubingwa Man
United, nani mwingine atakumbukwa? Wale ambao hawawezi kusahaulika ni wachezaji
waliofanya vizuri kimataifa na siyo England tu, watu kama kina Cristiano
Ronaldo, David Beckham, Lionel Messi, Zinedine Zidane na Ronaldinho. Hata
Galacticos. Ndio ni wachezaji wachache sana ambao hawawezi kusahaulika na wengi
wao wamechezea Real Madrid au Barcelona. Hivyo hii ni nafasi yake kwenda
Hispania na kuandika historia, kwa nini abaki England?
Je, Bale atakuwa na
subira kama Gerrard?
Ukimuuliza shabiki yeyote wa Spurs, jina gani linakuja
akilini ikitajwa Tottenham Hotspur, kuna jina moja tu. Pale White Hart Lane,
Bale anafanya kila kitu, lakini mpaka lini ataendelea kuwa hivi? Je, Bale
anaweza kuwa jeshi la mtu mmoja mpaka akifikisha miaka 30? Au atabaki kwa
misimu kadhaa kabla ya kuchoka?
Japo ni ngumu kwa mashabiki wa Liverpool
kukubali, lakini Steven Gerrard amefanya kila awezalo kuipa mafanikio timu
hiyo, lakini amegonga ukuta. Gerrard ameibeba timu yake ya utotoni miaka nenda
rudi bila taji la ligi kuu. Ndio pamoja na kukosa mataji, lakini nahodha huyo
wa Liverpool amevuna heshima, utiifu na kuungwa mkono. Lakini je, hayo
yatamtosha Bale? Siyo kila mchezaji anapata nafasi ya kujiunga na Real Madrid,
na itashangaza kukataa ofa hiyo, ambayo itamuwezesha kufikia malengo yake.
No comments:
Post a Comment