MADRID, Hispania
ATLETICO Madrid imetwaa taji lake la 10 la Copa del Rey, baada ya
mabao mawili kutoka kwa Diego Costa na Miranda kuwasaidia kuwafunga mahasimu
wao Real Madrid 2-1, katika muda wa nyongeza, fainali ambayo iliwashuhudia Jose
Mourinho na Cristiano Ronaldo wakionyeshwa kadi nyekundu.
Real Madrid ilikuwa haijafungwa kwa mechi 25 dhidi ya mahasimu wao
hao na kikosi hicho cha Mourinho kilianza vyema kwa bao la Cristiano Ronaldo,
aliyeunganisha kwa kichwa kona ya Luka Modric.
Lakini, Diego Costa alisawazishia Atletico dakika 10 kabla ya
mapumziko na Los Rojiblancos kisha wakanusurika hatari kadha baada ya mashuti
ya Mesut Ozil, Karim Benzema na Ronaldo kugongesha mwamba.
Mourinho alitolewa kwa kadi nyekundu dakika 77, kutokana na
kuonekana kugomea maamuzi na baadaye Miranda kufunga kwa kichwa kuifanya
Atletico kufunga bao la pili dakika nane baada ya muda wa nyongeza.
Kasheshe zaidi ilikuja baadaye, baada ya Ronaldo naye kutolewa kwa
kadi nyekundu baada ya kumchezea rafu Gabi, zikiwa zimesalia dakika sita tu
kabla ya filimbi ya mwisho.
"Tulipata nafasi mbili za wazi za kufunga, tuligongesha
mwamba mara tatu, hii ndiyo maana nasema haipo sawa," alisema Mourinho.
No comments:
Post a Comment