Sunday, May 19, 2013
FABREGAS ATAWEZA KUWA SCHOLES MPYA MAN UNITED?
MANCHESTER, England
PAUL Scholes ameona inatosha. Ameamua kung'atuka rasmi kwenye soka, lakini hii ikiwa ni mara ya pili, baada ya mwisho wa msimu wa 2010/2011 kuwahi kutangaza kutundika daluga zake kabla ya kurejea dimbani Januari ya mwaka jana, kujaribu kunusuru mambo katika klabu yake ya Manchester United.
Scholes awali alitangaza kung'atuka kwenye soka, lakini akiwa bado mwenye uwezo mkubwa kiuchezaji, hivyo baada ya United kuwa na tatizo la uhaba wa wachezaji wa kiungo na kocha Alex Ferguson alipomuomba arudi dimbani, kiungo huyo mwenye uwezo mkubwa alikubali kwa moyo mmoja kurudi dimbani kuendelea kuichezea timu ambayo anaipenda na ambayo ameichezea kwa miaka yake yote.
Aliporejea Scholes alileta mabadiliko makubwa kwenye kikosi cha United na kuweza kufukuzana na mahasimu wao Manchester City, wakiukosa ubingwa kwa tofauti ya mabao tu, baada ya timu hizo kufungana kwa pointi.
Scholes akasaini mkataba mwingine wa mwaka mmoja na kuichezea timu hiyo msimu huu na hatimaye kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu England, taji la 20 kwa klabu hiyo na taji la 11 kwa upande wake tangu alipoanza kuichezea timu hiyo yenye maskani yake Old Trafford.
Safari hii, Scholes ameamua kuondoka jumla. Ameamua kufuatana na kocha wake, Alex Ferguson, ambaye alitangaza kustaafu kuinoa timu hiyo baada ya kudumu kwa miaka 26 kwenye dimba la Old Trafford na sasa kocha wa Everton, David Moyes atarithi mikoba yake.
Lakini, wakati Scholes anaamua kurejea kwenye kikosi cha United, hilo lilitokana na timu hiyo kuwa na upungufu katika safu yake ya kiungo, kwasababu kwa kipindi hicho, Anderson, Tom Cleverley, wote hawa walikuwa wagonjwa na kusababisha Wayne Rooney alazimike kupangwa kwenye eneo hilo, huku Michael Carrick, akiwa ndiye mchezaji pekee wa eneo hilo aliyekuwa fiti kwa wakati huo.
Uhaba huo wa wachezaji viungo, ulisababisha Ferguson wakati mwingine alazimike kumtumia winga Antonio Valencia kama kiungo wa kati, jambo ambalo ni wazi kabisa liliigharimu timu hiyo ndani ya uwanja.
Scholes ni mchezaji wa klabu moja, hadi anang'atuka kwenye klabu yake hiyo ya Mashetani Wekundu, amecheza zaidi ya mechi 700 na taji la Ligi Kuu England walilotwaa msimu huu, lilihitimisha taji lake la 11 tangu alipoanza kuichezea klabu hiyo.
Na sasa Scholes anaondoka kwa mema kabisa na United inasaka mrithi wake, atakayechukua mikoba yake katika sehemu ya kiungo ya timu hiyo, ili kuifanya kuendelea kutamba nchini England na barani Ulaya kwa ujumla.
Nchini England, vyombo vya habari vimeanza kuvumisha mambo hasa katika kuelekea kipindi hiki cha usajili na kama kinachoelezwa kina ukweli, basi kiungo na nahodha wa zamani wa Arsenal, Cesc Fabregas, anatajwa kuwa mrithi rasmi wa Scholes katika kikosi cha United.
Nyota huyo wa kimataifa wa Hispania, Fabregas yupo kwenye mipango ya usajili wa mabingwa hao wa England, Man United, ambao wamepanga kwa nguvu zote kuboresha ubora wao katika sehemu hiyo ya kiungo.
United inataka kurekebisha baadhi ya mambo kwenye kikosi chake hasa baada ya Sir Alex Ferguson kuamua kustaafu, huku kukiwa na ripoti kwamba Wayne Rooney, naye anaweza kuondoka.
Kwenye kikosi cha United, pengo moja lililopo ni kiungo wa kati na tatizo hilo limeweza kudumu kwa misimu kadha ya hivi karibuni, kwamba wamekosa mchezaji mwenye uwezo mkubwa kwenye eneo hilo, ambaye angeweza kuwasaidia kutamba katika michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya.
Je, Cesc Fabregas ataweza kuwa mrithi sahihi wa Paul Scholes kwenye kikosi cha Manchester United?
Scholes atalipa soka kisogo jumla wakati wa majira ya joto, anaondoka akiwa shujaa kwa maana ya kunyakua medali zake 11 za ubingwa wa taji la Ligi Kuu England.
Uhamisho wa wachezaji kama Wesley Sneijder na Luka Modric, majina haya yamekuwa yakihusishwa na mpango wa kutua kwenye klabu hiyo kwa misimu kadha iliyopita, wakati United ilipokuwa ikimsaka kiungo mahiri wa kati, ambaye walau anaweza kurithi mikoba ya kiungo huyo wa zamani wa England.
Na sasa uhamisho wa Fabregas unaonekana kuwa ndio unaofaa hapa. Fabregas ni mchezaji mwenye uwezo wa kucheza sehemu ya kiungo goli hadi goli, mchezaji ambaye anaweza kuanzisha mashambulizi ya ushindi, mwenye nguvu na ubora, ambao ni wazi kabisa ndio inaoutafuta United ili kuweka mambo yao sawa.
Kutokana na nyota mwenzake wa zamani wa Arsenal, Robin van Persie, akiwa tayari ameshahamia kwenye kikosi cha United, uhamisho wa Fabregas ni kitu ambacho kinaweza kutimia kwenye kikosi hicho cha Old Trafford.
Cesc Fabregas ameshindwa kucheza kwa kiwango kikubwa tangu alipohamia Camp Nou kutoka Arsenal kwa uhamisho uliogharimu pauni milioni 35 mwaka 2011.
Baadhi ya mashabiki wa Barca, wamekuwa wakimshutumu Fabregas kwamba hachezi kwa kiwango bora, tofauti na alivyokuwa akikipiga katika kikosi cha Arsenal.
Lakini, mashabiki hao wa Catalan wamekuwa wakimshutumu Fabregas bila ya kutambua kwamba, kwenye klabu hiyo ya Barca na hata kwenye timu ya taifa, mara kwa mara amekuwa akitumika kama namba tisa bandia, badala ya kupangwa kiungo wa kati, mahali ambapo anapamudu zaidi.
Arsenal, sawa na klabu nyingine, hakika itaingia sokoni kusaka saini ya nyota wao huyo wa zamani kama wakitambua kwamba Barca inampiga bei, lakini United ni wazi kabisa uwezo wao wa fedha ni mkubwa na wataweza kushinda vita hiyo ya kumleta Old Trafford.
United inapewa nafasi kubwa ya kumsainisha kiungo huyo wa Hispania kama atakuwa tayari kuondoka La Liga. Iwe kama Fabregas atawekwa sokoni au la, hicho ni kitu kingine.
Kushuka kiwango chake cha zamani, hilo ni jambo la mpito tu, ubora wa kiwango chake utabaki kuwa juu daima na kwamba Fabregas hatatambulika kwa kiwango chake bora mahali kwingine duniani kama ataendelea kuwa Barcelona.
Mahali hapo, Fabregas hawezi kuonekana kuwa ni mchezaji mwenye ubora mkubwa, hasa akiendelea kufichwa na wakali wengine kama Xavi na Andres Iniesta, licha ya kwamba umri wao kwa sasa unaonekana kuwatupa mkono na Cesc atakuwa na nafasi ya kung'ara.
Fabregas na Thiago Alcantara watalazimika kusubiri ili waweze kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi hicho. Licha ya ukweli kwamba Barca imekiri kwamba, itafanya marekebisho makubwa katika kikosi chao mwishoni mwa msimu huu, Fabregas litakuwa dili safi kwa United na kwamba si kitu rahisi kwa kiungo huyo kuikataa jezi ya Man United msimu ujao.
Miamba hiyo ya Catalan, itahitaji kufanya marekebisho kadha, kwamba wachezaji kadha watajiunga na timu hiyo, lakini viungo wa kati si wachezaji waliokwenye orodha ya waliosokoni.
Nafasi ambazo timu hiyo ya Barca itahitaji kufanya marekebisho ni kipa, beki wa kati na mshambuliaji. Ubora wa Cesc Fabregas ni kitu kinachofikiriwa na Barca hawatahitaji kuachana naye, lakini ukweli wa mchezaji huyo ataweza kufanya mambo makubwa sana kama atatua Man United.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment