Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam imesema kuwa inaandaa barua ya kudai fidia ya Sh. bilioni 1.5 timu ya Azam kutokana na kitendo cha klabu hiyo kuwashitaki wachezaji wake wanne kwa madai kwamba walipokea rushwa ya Sh. milioni 7 ili wacheze chini ya kiwango katika mchezo uliozikutanisha klabu hizo ambapo Azam ilifungwa magoli 3-1.
Hatua hiyo ya Simba inafuatia taarifa iliyotolewa na TAKUKURU juzi ikieleza kwamba wachezaji wanne ambao ni Aggrey Morris, Deogratius Munishi 'Dida', Erasto Nyoni na Said Morad hawana hatia.
Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, alisema kuwa tayari klabu yake imeshawasiliana na mwanasheria wake baada ya kupata nakala ya hukumu iliyotolewa na TAKUKURU na wakati wowote kuanzia leo madai yao watayafungua kisheria.
Rage alisema kuwa wamefikia maamuzi hayo kutokana na klabu ya Simba kudhalilishwa katika jambo hilo katika kipindi chote tangu uongozi wa Azam ulipotangaza kwamba umewasimamisha wachezaji wake kwa kuwatuhumu wamepokea fedha jambo ambalo halikuwa kweli.
"Ni jambo la kuidhalilisha Simba na kutudhalilisha wana-Simba wote, hatuwezi kuliacha hivi hivi," alisema Rage.
WACHEZAJI WALIOSIMAMISHWA
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, nyota hao walisema kwamba wanasikia faraja kubainika hawana hatia na kwa sasa hawawezi kusema nini watafanya kwa sababu ni mapema mno.
"Mimi niko njiani natoka Zanzibar narejea Dar es Salaam, tutakapokutana wote pamoja ndiyo tutaamua hatua ya kuchukua, kwa leo ni mapema mno kusema chochote," alisema beki, Aggrey Morris jana mchana.
Jana jioni mmoja wa wachezaji hao aliliambia gazeti hili kwamba amepigiwa simu na kocha wa timu hiyo, Stewart Hall, ambaye amewataka leo asubuhi waonane na wahudhurie mazoezi.
KAULI YA AZAM
UONGOZI wa Azam ambao ulikuwa na kikao jana uliamua kuwarejesha katika timu wachezaji hao wanne ambao iliwasimamisha.
Katibu Mkuu wa Azam, Nassor Idrissa, alisema jana katika taarifa yao waliyoiweka kwenye tovuti ya klabu kwamba wanawakaribisha wachezaji hao kujiunga na timu kutokana na kutokutwa na hatia yoyote.
"Wachezaji hao wanakaribishwa rasmi kurudi kikosini Azam kwa ajili ya kujiunga na mazoezi na wachezaji wenzao," ilisema kwa kifupi sehemu ya taarifa ya klabu iliyotolewa jana saa 9 mchana.
Azam iliwasilisha barua ya malalamiko kwa TAKUKURU tangu Novemba 9 mwaka jana ikiwatuhumu nyota hao wanne kupokea rushwa kutoka Simba ili wacheze chini ya kiwango.
Mechi hiyo wanayotuhumiwa ilikuwa ya mzunguko wa kwanza wa ligi inayoelekea ukingoni sasa ambayo ilichezwa Oktoba 27 mwaka jana huku Azam ikiwa na machungu ya kuchapwa magoli 3-2 dhidi ya Simba kwenye mechi ya Ngao ya Jamii iliyofanyika Septemba 11 mwaka jana.
Licha ya kuwasimamisha nyota hao, Azam ilikuwa ikiendelea kuwapa mishahara wachezaji hao kama kawaida.
No comments:
Post a Comment