“NACHEZA
soka kwa sababu ni mchezo ninaoupenda ila hakuna manufaa niliyopata kuanzia
nianze kucheza zaidi ya kufanikiwa kununua fanicha tu”, ni maneno ya kiungo wa
kati wa Sayari Women na Twiga Stars, Fatuma Bushiri.
Katika
safari yake ya kucheza soka alianza kuchezea timu ya wanaume inayoitwa Papili
ya mtaani kwao Mwanayamala kwa Kopa wakati akisoma shule ya msingi
Mwananyamala.
Fatuma ambaye wasifu wake wa nje anafanana na
mwanaume kutokana na uvaaji wake na staili yake ya nywele (rasta) anasema
anatamani kama kanuni za ligi ya Tanzania ingeruhusu timu za kiume kusajili wachezaji wa kike ili siku moja acheze timu moja na Ramadhani Chombo
“Redondo” wa Simba kwani anapenda anavyocheza pindi awapo uwanjani.
Katika safari ya kucheza soka Fatuma anasema amekumbana na
mambo mengi ya kuhuzunisha na kufurahisha lakini hawezi kusahau mchezo wa kutafuta
kufuzu fainali za wanawake za Afrika kati ya Twiga Stars na Ethiopia.
Twiga ugenini jijini Addis Ababa ilifungwa na
wenyeji wao Ethiopia mabao 2-1, lakini ikiwa na matumaini ya kutumia vyema bao
la ugenini ilijikuta ikilala bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa katika mchezo wa
marudiano na hivyo kukosa tiketi ya kurudi tena kwenye fainali za wanawake
zilizokuwa zifanyike nchini Equatorial Guinnea.
Fatuma
ambaye ni kifungua mimba kwa mama Salma Abdallah mwenye watoto watatu alizaliwa Agosti 16, mwaka 1990 jijini Dar es salaam na alianza darasa la kwanza
mwaka 1998 na kuhitimu darasa la saba 2004 katika shule ya Msingi Mwananyamala.
Baada ya kushindwa
kuendelea na elimu ya sekondari kutokana na kipato cha wazazi wake
kutomudu kwani alilelewa na mama pekee
kwa sababu mama walitengana na baba yake alianza kujihusisha na kikamilifu
kwenye soka.
Timu ya
kwanza kumsajili ni Mndela Queens tangu mwaka 2006-2010 ambapo ilianza kushiriki ligi ya wanawake wilaya ya Kinondoni
na baadae ilipanda ligi ya Mkoa wa Dar es salaam kutwaa ubingwa wa ligi ya
wanawake 2010.
Licha ya
kuisaidia Mndela kutwaa ubingwa msimu mwaka 2011 aliipa kisogo Mndela Queens na
kujiunga na Simba Queens na kuisadia kuleta changamoto kwa vigogo wa soka la
wanawake, Sayari Women na Mburahati Queens na Simba ilifanikiwa kushika nafasi
ya tatu msimu wa 2011/2012.
Hata hivyo
hakudumu Simba Queens, badala yake alijiunga na Sayari Women ambayo ilikimbiwa
na nyota wake wengi kama Fatuma Omari na Sophia Mwasikili aliyesajiwa kucheza
soka la kulipwa Uturuki.
Kutokana na
kujituma kwake na kuzifumania nyavu kwa umaridadi aliitwa Twiga Stars tangu
mwaka 2006 hadi timu ilipoitwa mara ya mwisho mwaka jana.
Kiungo huyu
anasema pamoja na kuwa hakuna mafanikio makubwa kwenye soka la wanawake huwa
anaumia sana pindi timu inapofungwa hasa timu ya Taifa ya wanawake.
Anasikitika
sana kuona soka la wanawake halipewi kipaumbele kama soka la wanaume kwani kama
wangepewa sapoti Twiga Stars ingekuwa mbali.
“Sisi
wanawake hatupati sapoti kutoka kwa viongozi, tunaweza kuwepo uwanjani
tunafanya mazoezi ikija timu ya taifa ya wanaume tunaondolewa hata kabla ya
program ya kocha haijamalizika, hii inaonyesha jinsi soka la wanawake
linavyodharauliwa”, alisema Fatuma
Pia
anasisitiza kuwa pamoja na kutopewa
sapoti inavyotakiwa Twiga stars ndiyo timu ya soka nchini kucheza mashindano
makubwa kwani 2011 waliwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Olympiki
yaliyofanyika nchini Msumbiji, mashandano ambayo anakiri ndiyo waliyowahi
kupewa posho ambayo iliwaridhisha kidogo.
Mama yake
Fatuma anapinga sana uvaaji wa binti yake na staili yake ya nywele kwani
anamchukulia kama mhuni jambo ambalo Fatuma analipinga na anasononeka kuona
mama yake kutokubali staili yake.
“Mama yangu
ananisema kuhusu uvaaji wangu wa mavazi ya kiume na staili yangu ya nywele na
hapendi kuniona hivi lakini mimi najiona niko sawa”, alisema
No comments:
Post a Comment