Shirikisho
la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) limesema litaifungia Tanzania
iwapo itabainika kuwa Serikali imekuwa ikiingilia shughuli za Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
FIFA imesema kumekuwa na shutuma kupitia
taarifa mbalimbali za vyombo vya habari nchini kuwa Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo imeonesha nia ya kuingilia uendeshaji wa TFF.
Kwa
mujibu wa barua ya jana (Machi 10 mwaka huu) ya FIFA kwenda kwa Rais wa TFF,
Leodegar Tenga, vyombo vya habari vimemkariri Waziri (Dk. Fenella Mukangara)
kuwa Serikali imeiagiza TFF kutumia Katiba ya mwaka 2006 katika uchaguzi wakati
tayari imeshafanyiwa marekebisho.
“Pia imeelezwa kuwa TFF imetakiwa
kufanya Mkutano Mkuu pamoja na ule wa uchaguzi kwa tarehe ambazo zimepangwa na
Serikali. Vilevile imeelezwa kuwa Serikali inakusudia kuunda Kamati ya Muda
iwapo TFF haitatekeleza maagizo yake,” imesema sehemu ya barua hiyo iliyosainiwa
na Katibu Mkuu wa FIFA, Jerome Valke.
FIFA imesema iwapo yaliyoripotiwa
na vyombo vya habari yatathibitika kuwa kweli, maana yake huo ni uingiliaji wa
wazi wa Serikali kwa shughuli za TFF.
“Tunapenda kuwakumbusha kuwa
wanachama wote wa FIFA wanatakiwa kuendesha shughuli zao kwa uhuru bila
kuingiliwa na mtu mwingine kama ilivyoelezwa katika ibara za 13 na 17 za Katiba
ya FIFA.
“Hivyo kama maagizo hayo yanayodaiwa kutolewa na Serikali
yatatekelezwa, suala hili litapelekwa katika mamlaka za juu za FIFA kwa hatua
zaidi ikiwemo kuisimamisha Tanzania kama ambavyo inakuwa pale panapokuwa na
uingiliaji wa Serikali,” imesema barua hiyo.
Barua hiyo ambayo nakala
yake pia imetumwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) imeelezea baadhi ya
athari ambazo Tanzania itakumbana nazo endapo itasimamishwa ni timu za taifa
pamoja na klabu kutoshiriki mechi za kimataifa kwa mujibu wa Ibara ya 14 ya
Katiba ya FIFA.
Vilevile si TFF au wanachama wake na maofisa wengine
watakaoweza kunufaika na programu za maendeleo, kozi au mafunzo yanayotolewa na
FIFA na CAF.
“Madai ya uamuzi uliofanywa na Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo ni ya kusikitisha kutokana na ukweli kuwa FIFA
ilishatangaza itatuma ujumbe wake kuchunguza jinsi hali ilivyo kwa sasa na kutoa
mapendekezo yake. Kutokana na hali hii, ujumbe wa FIFA uliokuwa uje kuchunguza
(suala la uchaguzi) itabidi usubiri kwa vile ni muhimu kushughulikia tatizo hili
kwanza.
“Katika mazingira haya tunaomba ueleze msimamo huu wa FIFA kwa
mamlaka zinazohusika (Serikali) na athari ambazo mpira wa miguu wa Tanzania
utakumbana nazo. Tunakushuru na tunatarajia utatufahamisha kila hatua
inayoendelea katika suala hili,” imesema barua hiyo.
Boniface
Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
This comment has been removed by a blog administrator.
ReplyDeleteThis comment has been removed by a blog administrator.
ReplyDelete