KATIBU Mkuu wa Chama Cha Netiboli Tanzania, Rose Mkisi, amewataka wadau wa michezo kujitokeza kwa wingi leo kuchukua fomu mbalimbali kwa ajili ya kugombea katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Machi 24, mjini Dodoma.
Wakati Rose akiyasema hayo, jana saa tisa alasiri ndio ilikuwa mwisho wa kuchukua
fomu za uchaguzi huo, huku nafasi ya uenyekiti ikiwa imeombwa na mtu mmoja tu,
ambaye ni Anna Kibira.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Rose alisema nafasi ya
mwenyekiti hadi jana jioni ilikuwa imeombwa na mtu mmoja tu, hivyo kuonyesha
kuwa vado kuna umuhimu wa wanamichezo kujitokeza katika nafasi
mbalimbali.
Alisema kuwa wadau wamekuwa wazito kujitokeza katika kugombea nafasi
hizo kwa ajili ya kuhakikisha kuwa wanafanya kazi ya maana kuendeleza mchezo wa
netiboli hapa nchini.
“Ingawa muda unaelekea mwishoni, lakini mtu anaweza kuchukua fomu hapo
hapo pamoja na kuirudisha, ukizingatia kuwa hadi sasa wamejitokeza watu 11 tu
kwa kuwania nafasi za uongozi CHANETA,” alisema Mkisi.
Uchaguzi huo umepangwa kufanyika mkoani Dodoma mwishoni mwa mwezi huu,
huku mwenyekiti anayemaliza muda wake, Anna Bayi, akidaiwa kuwa hatatetea tena
nafasi yake kwa nia ya kuwapisha wengine waongoze, hasa kama hadi leo jioni
hatajitokeza katika kuchukua fomu hizo.
No comments:
Post a Comment