MJUE ABDALLAH ABDI KIJANA ALIYEANZA KUCHEZA DHUMNA AKIWA ANASOMA SEKONDARI
Abdallah Abdi kichanganya mabafa tayari kuanza kucheza mchezo |
“BARAZANI nyumbani kwetu kulikuwa na klabu yaFadhila ya
mchezo huu hivyo nikitoka shule nilikuwa nakaa naangalia jinsi wanavyocheza
baada ya wao kumaliza na wakirudisha vifaa ndani mimi napanga naanza kucheza”,
huu ulikuwa mwanzo wa mazungumzo yangu na Abdallah Abdi.
Abdi anasema alianza kucheza dhumna mwaka 1990 na mwaka
uliofuata alitokea kuwa mchezaji tegemeo kwenye klabu ya dhumna ya Fadhila
iliyopo mjini Tanga ambayo mwaka huo waliuwa mabingwa wa mkoa wa Tanga wakiwa
na wachezaji Musa Kishingo, Abeid na Anzuan.
“Wakati nasoma pia nilikuwa nacheza soka nikirudi nyumbani
jioni ndio naangalia jinsi wanavyocheza dhumna na baadae nikatokea kuwa
mchezaji tegemeo kwenye klabu ya Fadhila”, alisema Abdi ambaye hata hivyo
hadumu na klabu hiyo kwani alikwenda Arusha kwa ajili masomo ya Ufundi kwenye
chuo cha Ufundi Arusha ambacho kwa sasa kinatoa elimu ya Ufundi kwa ngazi ya
Chuo Kikuu
Akiwa Arusha mwaka 1992 alianzisha klabu iliyojulikana kama Revolution
ambayo alidumu nayo kwa muda wa miaka miwili kwani mwaka 1993 alihamia Dar es
Salaam.
“Baada ya kuanzisha klabu ya Revolution sikukaa nayo muda
mrefu kwani nilikatisha masomo na kuelekea Dar es Salaam kutafuta maisha”,
alisema kaka huyu mwenye lafudhi ya Kiswahili cha Pwani.
Nilipofika Dar es Salaam kwa sababu nilikuwa sina klabu
iliyosajili ili kuweza kushiriki mashindano ya wilaya ya Ilala nilisajiliwa
Tawaqal mwaka 1995 na aliisaidia klabu ya Tawaqal ilishika nafasi ya pili na
alipokuwa na klabu ya Mzizima na kucheza kwenye mashindano ya mkoa wa Dar es
Salaam, Mzizima ilishika nafasi ya tatu na bingwa ilikuwa klabu ya Idrisa ya
Magomeni.
“Nilisajiliwa na kucheza kwenye vilabu vya Tawaqal na
Mzizima kwa sababu klabu yetu ya Mafia tuliyoianzisha mwaka 1995 ilikuwa
haijapata usajili, na mimi ndie mwanzilishi wa klabu hii na ina vifaa vyote vya
mchezo wa dhumna”, alisema
Pia aliwataja waanzilishi wenzake kuwa ni Mzee Mwinyi Hamis
ambaye ni Mwenyekiti hadi sasa yupo, Ibrahim Musa ambaye ni nahodha, Masilahi Salum
Makamu Mwenyekiti, Faridi Hamis, Mzee Mageda na Said Bane hawa ni marehemu.
Baada ya kupata usajili waliendelea na mazoezi na mwaka 1998
walishiriki mashindano ya wilaya ya Ilala ambapo klabu yake iliibuka Bingwa na
kupewa kikombe na seti mbili za vifaa vya mchezo wa dhumna na Mh. Idd Zungu
ambaye ni mbunge wa jimbo la Ilala kupitia Chama cha Mapinduzi, mashindano
ambayo ndio ya mwisho kufanyika.
Abdallah Abdi ambaye ni Ofisa Utawala Mkuu wa Kampuni ya
Masoko Ltd, iliyopo jijini Dar es
Salaaam na baba wa watoto watatu ana waasa wachezaji washirikiane ili warudishe
hadhi ya mchezo huo ili uweze kupata wadhamini.
“Nawaasa wachezaji na vilabu vishirikiane ili kuupa hadhi
mchezo wa dhumna ili tuweze kupata wafadhili kama ulivyokuwa enzi za ufadhili
wa Suchak na Sas kwani ulipata umaarufu mpaka ukaimbwa kwenye taarabu”, alisema
Abdi.
Pia anasema raha ya mchezo wa dhumna inaonekana wakati
wanaocheza wanatamka majina ya mabafa mfano; bayadha, abaliyek,dubara, dusa,
duruji, dabashi, dusheshi, yek do, salim johari, besh shesh na nyinginezo.
Abdi ambaye alihitimu shule ya Sekondari ya Jumuiya mwaka 1991, anasema kamwe hatasahau siku ya
fainali za 1996 ngazi ya wilaya ya Ilala akiwa na klabu ya Tawaqal ambapo yeye
alikuwa mchezaji wa 10 na alitakiwa ashinde bao 3-0 ili klabu yake iwe Bingwa
lakini akiwa amefikisha ponti 99 mpinzani wake alifanikiwa kuchanga vema na
kushinda kwa bao 2-1.
“Kitendo cha kushindwa kwenye fainali hizo kiliniumiza sana
kwani niliaminiwa lakini nilipoteza kwenye dakika za mwisho na unajua mchezo ni
bahati ila sitakaa nisahau”, alisema Abdi.
Abdi ambaye alisoma shule ya Msingi ya msingi Lumumba jijini
Dar es Salaam kuanzia darasa la kwanza hadi la tano na baadae kumalizia shule
ya msingi Mabawa iliyopo Tanga anawashukuru wazazi wake, baba Abdi Juma na mama
Mwanaima Abdallah kwa malezi bora waliyompatia
kwenye elimu kidini na elimu dunia.
“Nimezaliwa kwenye
familia yenye watoto sita na nawashukuru wazazi wangu kwa malezi bora
waliyonipatia kwani imekuwa mwanga kuweza kuishi popote na watu wa aina
mbalimbali”, alisema
Pia alisema pamoja na kuwa dhumna haina kipato kama mchezo
wa soka ila ni mchezo mzuri ambao unajenga akili anawaomba viongozi kusimamia
vema mchezo huu kwa kuanzisha mashindano kama ilivyokuwa miaka ya tisini.
“Pamoja na kuwa mchezo huu unachezwa sana sehemu za pwani si
mchezo wa magoigoi na ndio maana unachezwa mara nyingi kuanzia jioni muda ambao
kila mtu keshatoka kwenye mihangaiko ya kutwa”, alisema
Abdi ametoa wito kwa serikali na viongozi kutoa fursa sawa
kwa michezo yote ili kusaidia kuinua michezo yote ipate kujulikana na watu
kwani kuna michezo iliyosahaulika kama dhumna.
No comments:
Post a Comment