Kocha Mubaraka Hassan akitoa maelekezo kwa mchezaji |
MUBARAKA HASSAN KOCHA MWENYE HISTORIA NZURI NA ASHANTI UNITED
Aliipandisha ikaiacha ikashuka
daraja na sasa ameipandisha tena
“SOKA ni mchezo wenye mashabiki wengi duniani kote na hata
Tanzania unaongoza pia lakini wachezaji wa siku hizi hawautendei haki mchezo
huu”, huu ulikuwa ni mwanzo wa mazungumzo yangu na kocha Mubaraka Hassan
Ni kocha mwenye sura ya upole
lakini mkali akiwa kwenye kazi kwani hata aje mchezaji ambaye ameshindikana
kwenye timu nyingine kwake lazima atafuata maelekezo yake ipasavyo lakini
anasema kamwe hatasahau alipoteguka mkono wakati akicheza mpira kwenye uwanja wa Msimbazi
Rovers na wachezaji wenzake wa timu ya Msimbazi Mission, wakamrudisha nyumbani
akaenda kupelekwa hospitali ya Muhimbili na mama yake.
Anasema kuwa enzi wakicheza soka
walikuwa wanajitoa kwa sababu wachezaji walikuwa wana mapenzi ya dhati na timu
wanayochezea kamwe huwezi kumkuta mchezaji anachezea timu ambayo hana mapenzi
nayo lakini siku hizi wanafuata pesa na marupurupu.
Pia anatabainisha kuwa hata
vilabu vya Simba na Yanga vilikuwa vinasajili wachezaji ambao wana mapenzi ya
kweli na klabu yao na ilikuwa nadra kumkuta mchezaji msimu huu akiwa anachezea
Simba na Msimu ujao ukamkuta anachezea Yanga. Anaendelea kusema kuwa Yanga
walikuwa wanachekua wachezaji kwenye timu ya African ya Temeke na Simba
walikuwa wanachukua kwenye Good hope ya Temeke pia
Mubaraka amechezea timu nyingi
katika mikoa mbalimbali nchini Tanzania lakini alimalizia soka lake kwenye timu
za Pentagon ya Ilala na Dandee United ya
Dodoma.
“Siku hizi wachezaji wanafuata
pesa tu kwenye vilabu wanavyochezea kwani uchezaji wao uwanjani haulingani na
pesa wanazolipwa tofauti na enzi zetu tunalipwa kidogo lakini mtu anajitoa
kiukweli”
Alianza kufundisha “ukocha’ mwaka
1995 baada ya kuamua kutundika daruga kwani alikuwa kiungo namba nane wa
kutegemewa licha ya kuwa soka lake lilishia daraja la kwanza.
Timu ambazo amewahi kuzifudisha
kwa vipindi tofauti ni Peshico, Pentagon, Mkunguni, Cosmo Politan, Manyema na
Ashanti United zote ni za Ilala ila anasema Ashanti ndio timu ambayo ana
historia ndefu nayo.
“Ashanti ni timu pekee ambayo
naweza kusema nina mafanikio nayo kwani nilianza kuifundisha mwaka 2004
ikafanikiwa kuingia Ligi Kuu mwaka 2005 nikaicha ikashuka daraja na sasa
niliichukua tena kuanzia mwaka 2012 na mwaka huu imefanikiwa kuingia tena Ligi
Kuu”, alisema Mubaraka huku akitabasamu.
Mubaraka anasema kuwa wakati
alipoipandisha Ashanti United Ligi Kuu mwaka 2005 aliendelea kuifundisha na
ikafanikiwa kuleta changamoto kwenye ligi kuu kwa misimu mitatu aliyokuwa nayo
kwenye ligi Kuu lakini mwaka 2008 aliondoka Ashanti na msimu huo Ashanti
ikashuka daraja.
Pia anasema baadaye Ashanti
ilicheza ligi daraja la kwanza msimu mmoja tu ambao ni mwaka 2009 na misimu
miwili timu ilipumzika baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kubadilisha
kanuni za kuendesha ligi kwa kuondoa madaraja na kuingiza ligi kwa mfumo ngazi
ya wilaya, mkoa na taifa.
Mfumo ambao msimu huu umefutwa na
kurejeshwa ule wa zamani wa madaraja jambao ambalo Mubaraka anasema ndio mfumo
mzuri kwa kuendeleza soka kwani haiwezekani timu ishuke kutoka Ligi Kuu iende
hadi ngazi ya wilaya ikaanze kushindana upya kutafuta kupanda tena.
“Timu ikishuka kutoka ligi kuu
inakwenda hadi ngazi ya wilaya inakuwa vigumu tena kwa timu kujipanga kurudi
tena na mfumo huo ulipoteza timu nyingi kama hazikuwa na mipango thabiti”,
alisema
Baada ya Ashanti kupumzika kwa
miaka miwili, Mubaraka alianza tena kuifundisha mwaka 2012 akianzia ngazi ya
wilaya, ikachukua ubingwa wa wilaya ikafanikiwa kucheza ligi ya Kanda kwa Mkoa
wa Dar es Salaam, safari hii ikapenya tena ikiwa miongoni mwa timu tatu
zilizoingia ligi daraja la kwanza zikitokea Dar es Salaam.
“Ligi ya Kanda Mkoa wa Dar es
salaam ilikuwa ngumu lakini kulingana na jinsi nilivyowafundisha wachezaji na
kujenga nidhamu ilinisaidia kufanikiwa kuingia ngazi ya kituo ambayo ilikuwa
Musoma na huko ndio kulikuwa na uzalendo wa hali ya juu kwani bila nidhamu
niliyokuwa nasisitiza hasira zilizotokana na kuonewa na waamuzi zingeweza
kabisa kufanya timu kuondolewa kwenye mashindano.
Tulifanikiwa kupenya kwenye kituo
na kuingia Ligi daraja la Kwanza, kwa kuwa na nidhamu na wachezaji wenye
kufuata maelekezo yangu. Nilijitahidi kuibadilisha Ashanti kwani kuna sifa
ambayo ilikuwa imeenea miongoni kwa baadhi ya wadau kuwa wachezaji wa timu ya
Ashanti ina nidhamu mbaya na sikutaka iwe hivyo kwani malengo yalikuwa ni
kufika ligi kuu na tunamshukuru Mungu tumefanikiwa kabla hata hatujamaliza
ligi”, alisema Mubaraka huku akitoa pongezi kwa uongozi wa Ashanti kwa sapoti
kubwa kwao na mashabiki.
Mubaraka anasema kuwa Ashanti
ikiwa daraja la kwanza kwenye kundi B, imecheza michezo 12, imeshinda michezo 8
na imetoka sare michezo 4 ina pointi 28 na imebakisha michezo 2 na mpaka sasa
hakuna mchezaji yeyote aliyeonyeshwa kadi nyekundu.
Pointi 28 ilizonazo hakuna timu
yeyote itakayozifikia kwani wapinzani wao Villa Squad ya Kinondoni ina pointi
20 na ikifanikiwa kushinda michezo miwili iliyobakia itakuwa na pointi 26 tu.
Mubaraka anasema pamoja na
kucheza soka na kufundisha hakuna mafanikio yeyote ambayo anaweza kusema
yametokana na mpira zaidi ya kuwa maarufu tu mjini lakini anatoa wito kwa
makocha wengine waige mfano wake kwa kujitolewa kufundisha vilabu vya huku
chini ili kuinua soka la Tanzania na kuendeleza kipaji chao kwani kufundisha
inasaidia kujenga ubunifu wa ufundishaji (skills).
“Sina mafanikio yeyote ambayo
naweza kusema yametokana na mpira ila nashukuru umeniweka karibu na watu wengi
na nimefahamika pia lakini nawaasa makocha wenzangu waache kukimbilia vilabu
vikubwa kwa sababu ya maslahi wasaidie pia vilabu vidogo ili kujenga timu bora
na wachezaji wenye kujua soka”, alisema Mubaraka.
Kocha huyu mwenye mke na watoto
wane mmoja akiwa mvulana anasema kuwa wachezaji watumie vipaji vyao kwenye soka
na kujituma zaidi si kuchanganya vipaji viwili huku akimtolea mfano Ali Kiba
ambaye ni mchezaji mzuri na mwanamziki pia lakini amebaki kwenye mzuki kwani
ndio kwenye mafanikio zaidi.
Pia anasisitiza wachezaji,
makocha na viongozi wa soka wawe na uzalendo wa kweli katika soka ili kusaidia
kuendeleza soka la Tanzania
No comments:
Post a Comment