Blogroll

KWA MAWASILIANO ZAIDI TUWASILIANO KUPITIA BARUA PEPE pallangyorachel@yahoo.com AU NIPIGIE KUPITIA NAMBARI 0715187511

Pages

Tuesday, February 12, 2013

TFF YAWASIHI MASHABIKI KUZISHANGILIA SIMBA NA AZAM

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linawataka mashabiki wa mpira wa miguu kujitokeza kwa wingi wikiendi hii kuzishangilia timu za Azam na Simba zitakazocheza mechi za mashindano ya Afrika jijini Dar es Salaam.

Nguvu ya washabiki ni muhimu katika kuziweza timu hizo kufanya vizuri katika mechi hizo za nyumbani dhidi ya Al Nasir Juba ya Sudan Kusini na Club Libolo ya Angola.

Azam itacheza Jumamosi (Februari 16 mwaka huu) dhidi ya Al Nasir katika mechi ya Kombe la Shirikisho wakati Simba itaikabili Club Libolo kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayofanyika Jumapili. Mechi zote zitachezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

LYON, YANGA KUUMANA UWANJA WA TAIFA
Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania ubingwa wa Tanzania Bara inamaliza raundi ya 16 kesho (Februari 13 mwaka huu) kwa mechi kati ya wenyeji African Lyon dhidi ya Yanga itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mechi hiyo itakayochezshwa na mwamuzi Martin Saanya kutoka Morogoro inakutanisha timu zenye mazingira tofauti. Wakati Yanga wakiwa ndiyo vinara wa ligi hiyo kwa pointi 33, African Lyon ambayo sasa inanolewa na Salum Bausi inakamata mkia ikiwa na pointi tisa tu.

Nayo Toto Africans itaikaribisha Polisi ya Morogoro kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza katika mechi itakayochezeshwa na mwamuzi Jacob Adongo kutoka Musoma. Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 20,000 utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Mgambo Shooting na Oljoro JKT.

Nahodha wa zamani wa Taifa Stars, Mecky Maxime ambaye sasa ni kocha wa Mtibwa Sugar ataiongoza timu yake hiyo katika mechi dhidi ya Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Manungu ulioko Turiani, Morogoro. Ni kwenye uwanja huo huo ambapo Mtibwa Sugar katika mechi yao iliyopita walichapwa mabao 4-1 na Azam.
                     
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment