WANAFUNZI 90 WA SAYANSI NA TEKNOLOJIA WATUA ALGERIA KUSAKA SHAHADA



Jumla ya wanafunzi 90 wa Tanzania waliopata ufaulu wa juu katika masomo ya afya, sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM) wamewasili nchini Algeria kuanza masomo ya shahada katika vyuo vikuu mbalimbali nchini humo, chini ya ufadhili wa Programu ya Samia Scholarship.

Wanafunzi hao waliwasili jioni ya tarehe 24 Novemba 2026 kwa ndege ya Shirika la Ndege la Qatar na kupokelewa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Houari Boumedienne jijini Algiers na Balozi wa Tanzania nchini Algeria, Mobhare Matinyi, pamoja na maofisa wa Ubalozi na watendaji wa Wizara ya Elimu ya Juu na Utafiti wa Kisayansi wa Algeria.

Akizungumza na wanafunzi hao tarehe 25 Novemba 2026 katika Chuo Kikuu cha Blida, kilichopo kilomita 45 kutoka Algiers kabla ya kuelekea kwenye vyuo walivyopangiwa, Balozi Matinyi amewataka kusoma kwa juhudi na bidii wakitambua kuwa wao ni ndoto na fahari ya taifa. Amewasisitiza kuishi kwa ushirikiano na kudumisha heshima ya nchi na ya ufadhili huo.





Mkurugenzi wa Elimu ya Juu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Steven Maluka, aliyeongoza msafara huo, amebainisha kuwa hii ni mara ya kwanza kwa serikali kugharamia kundi kubwa la wanafunzi bora 90 kwenda nje ya nchi kusomea shahada za sayansi na teknolojia, huku akimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zilizowezesha fursa hiyo.

Katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Chuo Kikuu cha Blida, Profesa Bachir Amer, aliwasilisha salamu kutoka kwa Waziri wa Elimu ya Juu na Utafiti wa Kisayansi wa Algeria, Profesa Kamel Bidari. Ujumbe wa serikali uliowasindikiza wanafunzi pia uliwajumuisha Afisa Mwandamizi wa Wizara, Daktari Fabian Nyenyembe, na Mratibu wa Samia Scholarship, Profesa Liliane Pasape kutoka Chuo Kikuu cha Nelson Mandela (NM-AIST) cha Arusha.

Wanafunzi hao wamegawanywa katika vyuo vikuu bora nchini Algeria vikiwemo Algiers, Annaba, Batna, Blida, Boumedienne, Boumerdes, Chlef, Constantine, Mostaganem, Oran, Setif, Sidi Bel Abbes, Skikda na Tiaret, ambapo pamoja na masomo yao ya taaluma, watapata fursa ya kujifunza lugha za Kifaransa au Kiarabu.

No comments