TANZANIA KUENDELEA KUTOA WATAALAMU OPERESHENI ZA AMANI ZA UMOJA WA MATAIFA
Aidha aimesema
itaendelea kutoa wataalamu wenye weledi na taaluma mbalimbali kwa ajili ya
kushiriki katika operesheni za ulinzi wa Amani za Umoja wa Mataifa.
Kauli
hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mhandisi Hamad
Yussuf Masauni, wakati alipomwakilisha
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi,
katika maadhimisho ya Siku ya Polisi wa Umoja wa Mataifa, yaliyofanyika Dar es
Salaam leo Novemba 29, 2026.
Mhe.
Masauni amesema Tanzania inajivunia historia yake ya muda mrefu ya kushiriki
katika operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa na imedhamiria
kuendelea kutoa askari na wataalamu wenye sifa, weledi na kujitolea kwa ajili
ya kuhudumia chini ya bendera ya Umoja wa Mataifa.
Amesema
ushiriki wa Polisi wa Umoja wa Mataifa katika maeneo mbalimbali yanayokabiliwa
na migogoro una mchango mkubwa katika kurejesha utulivu, kuimarisha utawala wa
sheria, kulinda raia na kujenga imani ya wananchi kwa taasisi za usalama.
“Tunatoa
pongezi na shukrani za dhati kwa askari wote wa Polisi wa Umoja wa Mataifa,
waliopo kazini na waliowahi kulitumikia jukumu hili, kwa mchango wao mkubwa
katika kudumisha amani na usalama wa kimataifa,” amesema Mhe. Masauni.
Ameeleza
kuwa dunia inakabiliwa na changamoto mbalimbali, zikiwemo shinikizo la kiuchumi
na kifedha linaloathiri mataifa pamoja na taasisi za kimataifa, lakini
amesisitiza kuwa juhudi za kutafuta na kudumisha amani zinapaswa kuendelea kuwa
kipaumbele cha pamoja.
“Amani
ndiyo msingi wa maendeleo, ustawi wa jamii na kulinda utu wa binadamu, hivyo ni
muhimu Umoja wa Mataifa na nchi wanachama kuendelea kuunga mkono operesheni za
ulinzi wa amani na juhudi za kujenga amani katika maeneo mbalimbali duniani.”
Kwa
upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Patrobas Katambi, amesema
Tanzania ina heshima kubwa katika Umoja wa Mataifa iliyojengwa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambayo
imesababisha kufanyika kwa kikao hicho cha Vyuo vinavyohusika na masuala ya
Usalama na Amani Duniani.
Amesema
kikao hicho cha mwisho wa mwaka kilihusu masuala mbalimbali ikiwemo ushiriki wa
Vyombo vya Ulinzi na Usalama, hususan Polisi, kuhakikisha amani inaendelea
kutawala hasa maeneo yenye migogoro.
Ameongeza
kuwa msingi wake ni kuendeleza usalama na amani na nchi wanachama wanashiriki
ikiwa ni pamoja na jukumu la kujenga uwezo kwa Vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa
nchi husika pamoja na kutoa elimu.
Awali,
Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Camillus Wambura, alisema Jeshi la Polisi
limeendelea kuwa karibu na jamii na kuhakikisha linafanya kazi yake kwa weledi
ili amani iendelee kuwepo.
Katika
maadhimisho hayo, Tanzania imeeleza heshima yake kwa kuchaguliwa kuwa mwenyeji
wa mkutano huo muhimu unaowakutanisha viongozi wa kimataifa, wataalamu wa
ulinzi wa amani na maafisa wa Polisi wa Umoja wa Mataifa kutoka maeneo
mbalimbali duniani.



Post a Comment