Meli ya Kitalii 'Emerald Kaia' Yatia Nanga Kilwa: Watalii Wapagawishwa na Urithi wa Dunia
Meli ya kitalii ya Emerald Kaia imetia nanga katika Bandari ya Kilwa mkoani Lindi ikiwa imebeba zaidi ya watalii 70 kutoka mataifa mbalimbali duniani, ikiwemo Scotland, Ireland, Ujerumani na Austria.
Watalii hao wapo nchini kujionea utajiri wa urithi wa kihistoria na utamaduni nchini.
Ujio wa meli hiyo unafungua rasmi msimu wa utalii katika visiwa vya Kilwa.
Watalii hao wanatarajiwa kujifunza historia ya magofu ya kale pamoja na kutembelea maeneo yenye hifadhi ya ndege wa aina mbalimbali.
Akizungumza wakati wa mapokezi hayo, Afisa Utalii kutoka Mamlaka ya Uhifadhi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Bi. Ruth Palangyo, ameeleza kuwa ujio huo ni mwanzo tu, kwani wanasubiri meli nyingine kadhaa za kitalii zinazokuja kwa ushirikiano na wadau wa sekta hiyo.
Watalii Wafunguka Wanachoshangaa
Watalii waliofika katika eneo hilo wameonyeshwa kuvutiwa sana na utunzwaji wa majengo ya kale, huku wakiahidi kuwa mabalozi wa kutangaza vivutio hivyo pindi watakaporejea makwao.
Mmoja wa watalii hao alisema kuwa amekuwa akitembelea Tanzania mara kwa mara kwa ajili ya utalii wa wanyamapori (safari), lakini safari hii imempa picha tofauti kabisa: "Nimeona upande mwingine wa kipekee wa Tanzania, hasa jinsi urithi huu wa dunia unavyolindwa na kuhifadhiwa kwa kiwango cha juu."
Mtalii mwingine aliongeza kuwa, ingawa hali ya hewa ina joto ambalo hawakuzoea, ukarimu wa watu, historia na utamaduni mzuri umefanya ziara hiyo kuwa ya kukumbukwa mno.
Alimalizia kwa kutoa rai kwa watalii wengine duniani kote kutembelea Tanzania ili kujionea maajabu haya ya kihistoria.





Post a Comment