RICK ROSS AMMWAGIA SIFA RAIS SAMIA




Msanii nguli wa muziki wa Hip-hop kutoka Marekani, William Roberts, anayefahamika zaidi kama Rick Ross, amempongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za dhati za kuendelea kuweka Tanzania kwenye ramani ya dunia, huku akisisitiza kuwa muziki na vipaji vinavyotoka nchini vinapaswa kupewa nafasi kubwa zaidi katika jukwaa la kimataifa.

Katika ujumbe wake uliosambaa kupitia mtandao wa kijamii ukiwa na picha za mjongeo, Rick Ross alieleza kuwa Tanzania imekuwa kwenye mawazo yake kutokana na ukubwa wa vipaji vya muziki na hamasa kubwa inayotoka ndani ya nchi hiyo.

"Heshima kubwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuiweka Tanzania kwenye ramani ya dunia," alisema msanii huyo.

Mbali na sifa hizo, Rick Ross alizungumzia uzuri wa kipekee wa Tanzania akitaja vivutio maarufu vya Serengeti na Zanzibar, huku akiweka wazi utayari wake wa kuitembelea nchi hiyo ili kutumia muda mwingi kukutana na wananchi wake, kufahamu utamaduni wao, na kupata uzoefu wa moja kwa moja wa maisha ya Kitanzania.

Aidha, msanii huyo alifichua kuwa yeye na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, wana mipango mikubwa ya kushirikiana kuinua tasnia ya muziki nchini. Mipango hiyo inajumuisha kufanya kazi na baadhi ya wasanii wakubwa wa Tanzania pamoja na kuwafikia wasanii wa kizazi kipya na chipukizi ili uwezo wao mkubwa uweze kushuhudiwa na dunia nzima.

No comments