JAJI MKUU GEORGE MASAJU ASISITIZA USHIRIKIANO WA TAASISI ZA HAKI JINAI



Jaji Mkuu wa Tanzania, George Masaju, amesisitiza kuwa mfumo wa haki jinai si mali ya taasisi moja pekee, bali ni mkusanyiko wa viungo vinavyotegemeana ambapo udhaifu wa sehemu moja huathiri moja kwa moja ufanisi wa mfumo mzima wa utoaji haki nchini. 

Akifunga mkutano wa Mahakama na wadau wa haki jijini Dodoma uliolenga kuimarisha ushirikiano na mahusiano katika utekelezaji wa majukumu, Jaji Mkuu alifananisha taasisi hizo na viungo vya mwili na kueleza kuwa hakuna taasisi inayopaswa kujiona bora kuliko nyingine katika kusimamia utawala wa sheria na ulinzi wa amani kwa mujibu wa Katiba.

Akifafanua mtiririko mzima wa mnyororo huo, Jaji Masaju alieleza kuwa safari ya haki huanzia ndani ya jamii tukio linapotokea, kisha kupita mikononi mwa vyombo vya uchunguzi kama vile Jeshi la Polisi, TAKUKURU, na DCEA kabla ya kufikishwa katika Ofisi ya Taifa ya Mashitaka na hatimaye mahakamani, huku akionya kuwa Mahakama haiwezi kufikia ufanisi wa asilimia mia moja iwapo hatua za mwanzo kama vile ukamilishaji wa uchunguzi, upatikanaji wa mashahidi, na uwasilishaji wa jalada kwa wakati zitakabiliwa na makwamo. 

Alihimiza matumizi mapana ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na mifumo inayounganisha taasisi hizo ili kuondoa urasimu na kuharakisha upatikanaji wa haki kwa usawa na uadilifu.

Aidha Jaji Mkuu alikumbusha misingi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayoweka mbele amani, usalama, na uimara wa taasisi kama nguzo kuu za utawala bora, huku akizitaka mamlaka zote za mnyororo wa haki jinai kujiandaa mapema kukabiliana na athari za mvua za El Nino kwa kuimarisha miundombinu yao ili kuhakikisha huduma kwa wananchi hazikatiki hata wakati wa majanga ya kimaumbile..

No comments