PSSSF YATAKA WASTAAFU KUTUMIA MIFUMO KUEPUKA MATAPELI

 



Na Marco Maduhu, SHINYANGA

 

WASTAAFU nchini wametakiwa kuwa makini na watu wanaojitambulisha kama mawakala wa Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), wakihimizwa kutumia njia rasmi za mifumo ya kidijiti ya mfuko huo kuhakiki taarifa zao na kufuatilia mafao yao.

Tahadhari hiyo imetolewa leo, Septemba 18, 2026, na Afisa Msimamizi wa PSSSF Mkoa wa Simiyu, Salum Mwegelo, wakati wa semina ya PSSSF kwa waandishi wa habari wa Mtandao wa Wanablogu Tanzania (Tanzania Bloggers Network – TBN) na Klabu za Waandishi wa Habari za Shinyanga na Simiyu.

Mwegelo amesema baadhi ya wastaafu wamekuwa katika hatari ya kutapeliwa kutokana na kutumia watu wasio rasmi wanaodai kuwa wanaweza kuwasaidia katika taratibu za kuhakiki taarifa, kufuatilia au kupata mafao yao.

Amesema watu hao wanaweza kuomba taarifa nyeti za wastaafu, ikiwemo namba za siri za akaunti za fedha na taarifa nyingine binafsi, ambazo zinaweza kutumiwa kufanya miamala bila ridhaa ya wahusika.

Mwegelo amesisitiza kuwa PSSSF haina mawakala wanaotoa huduma kwa niaba ya mfuko huo, hivyo wastaafu wanapaswa kuwa na tahadhari dhidi ya mtu yeyote anayejitambulisha kama wakala wa PSSSF na kuwaomba taarifa zao za siri.

Amesema wastaafu wanapaswa kutumia njia rasmi zinazotolewa na PSSSF, ikiwemo kufika katika ofisi za mfuko huo au kutumia mifumo ya kidijitali inayowawezesha wanachama na wastaafu kufuatilia na kuhakiki taarifa zao kwa usalama.

Amesema matumizi ya mifumo ya kidijitali ni miongoni mwa njia zinazoweza kuwasaidia wanachama kupata taarifa zao kwa urahisi bila kulazimika kuwapa watu wengine taarifa zao binafsi au za kifedha.

Kwa upande wake, Afisa Uhusiano wa PSSSF, Abdul Njaidi amewataka waandishi wa habari na wanablogu kutumia taaluma yao kuwafikishia wananchi taarifa sahihi kuhusu huduma za mfuko huo, hususan elimu inayohusu haki, wajibu na taratibu za kupata mafao.

 


Njaidi amesema vyombo vya habari, blogu na majukwaa ya kidijitali vina nafasi kubwa katika kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wanachama na wastaafu kwa lugha rahisi na inayoeleweka, huku akiwataka waandishi na wanablogu kuthibitisha taarifa kabla ya kuzifikisha kwa umma.

Amesema elimu sahihi inaweza kusaidia kuwawezesha wanachama na wastaafu kutambua njia halali za kupata huduma za PSSSF na kuchukua tahadhari dhidi ya watu wanaoweza kutumia mwanya wa ukosefu wa taarifa kuwahadaa.

Mratibu wa Tanzania Bloggers Network (TBN) Kanda ya Ziwa, Kadama Malunde, amepongeza PSSSF kwa kuandaa semina hiyo, akisema mafunzo kama hayo ni muhimu kwa waandishi wa habari na wanablogu kwa kuwa yanawaongezea uelewa wa masuala wanayopaswa kuyafikisha kwa jamii.



Malunde amesema waandishi na wanablogu wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha kila taarifa wanayoitoa kwa umma inathibitishwa, ina usahihi na inatoka katika vyanzo vinavyoaminika, hususan katika kipindi hiki ambacho taarifa za kidijitali zinaweza kusambaa kwa kasi kubwa.

“Semina kama hii ni muhimu kwa sababu inatupa nafasi ya kujifunza na kuongeza uelewa. Tukiwa waandishi na wanablogu, jukumu letu si kuchapisha taarifa tu, bali kuhakikisha taarifa tunazowafikishia wananchi ni sahihi, zimehakikiwa na zina manufaa kwa jamii,” amesema Malunde.

Naye Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga, Greyson Kakuru, amesema semina hiyo imekuwa na umuhimu mkubwa kwa waandishi wa habari na wanablogu kwa kuwa imewapa uelewa zaidi kuhusu huduma za PSSSF na masuala yanayowahusu wanachama na wastaafu.

Kakuru amesema maarifa yaliyopatikana yatawasaidia waandishi na wanablogu kuandaa na kusambaza habari zenye usahihi, huku wakitoa elimu kwa jamii kuhusu namna ya kutumia huduma za PSSSF na kujilinda dhidi ya utapeli.

No comments