Hili la Waziri Mkuu linaswihi, tuzike ushabiki wa ndani na kusimama na wawakilishi wetu
Soka la klabu kwa sasa sio tena suala la burudani ya wikendi ya kupotezea muda; ni nyenzo kuu ya diplomasia ya kiuchumi, mshikamano wa kijamii, na mtaji wa kisiasa kwa taifa lolote linalotaka kusikika duniani. Ndio maana rai ya viongozi kama Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ya kuwataka Watanzania kuweka kando ushabiki wa Simba na Yanga na kusimama kidete nyuma ya wawakilishi wetu kimataifa inapaswa kutazamwa kwa jicho pana la kizalendo na kiuchumi.
Ukitazama wito huu unazihusu klabu zote nne zinazobeba bendera ya nchi msimu huu: Simba SC, Young Africans , Azam FC, na Singida Black Stars.
Katika mtazamo wa kijamii, ushabiki wa klabu nchini umegawanyika kwa misingi ya kiushindani ambayo mara kwa mara huzaa uhasama wa ndani usio na tija. Utamaduni wetu umetekwa na sumu ya "kila mtu na chake." Mwalimu mstaafu wa shule ya msingi huko Tandika, ambaye ni shabiki damu wa Simba, aliwahi kukiri wazi bila hofu kuwa angependelea Yanga ipigwe mabao matano ugenini dhidi ya Mamelodi Sundowns kuliko kuona inasonga mbele.
Huo ni mfano hai wa jinsi uhasama wa ndani unavyofifisha uzalendo wa kimataifa. Kisaikolojia, jamii yetu imegawanyika kiasi kwamba tunasherehekea anguko la mwenzetu hata kama aangukaye anaiwakilisha bendera ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Dkt. Mwigulu Nchemba alipomsisitiza Spika Idd Azzan Zungu—ambaye anafahamika kwa itikadi yake ya Simba—kushabikia timu pinzani kimataifa, alikuwa anagusa jeraha hili la kijamii kwamba utambulisho wetu kama taifa unapaswa kuwa mkubwa kuliko ukuta wa rangi za njano na kijani au nyekundu na weupe.
Ndio kusema pale timu zinapovuka mipaka ya nchi, uwanja unabadilika na kuwa jukwaa la utambulisho wa kitaifa (national identity), ukijenga "fahari ya pamoja" na kuvunja kuta za matabaka au itikadi.
Tanzania inashika nafasi nzuri kwenye viwango vya ubora vya Shirikisho la Mpira Miguu Barani Afrika (CAF), jambo ambalo linaipa fursa ya kutoa timu nne (mbili kwenye Ligi ya Mabingwa na mbili Kombe la Shirikisho) katika michuano ya kimataifa ya klabu.
Katika ramani ya soka la Afrika, nchi imejijengea heshima kubwa huku klabu zake zikiwa kwenye hatua za awali za kusaka tiketi ya kutinga hatua ya makundi. Simba SC na Yanga zinawakilisha nchi kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, zikianza kampeni zao katika hatua ya kwanza ya mchujo dhidi ya Mighty Wanderers ya Malawi na Gaborone United ya Botswana, wakati Azam FC na Singida Black Stars zinapambana vikali kupeperusha bendera ya nchi kwenye Kombe la Shirikisho.
Rai ya kuweka kando ushabiki wa klabu za ndani wakati timu za Tanzania zinaposhiriki kimataifa ni nguzo muhimu ya kujenga uzalendo wa kweli. Kwanza, uwakilishi wa kimataifa hauhusu tena klabu binafsi, bali unahusu Taifa lenyewe. Kila ushindi unaopatikana unachangia alama za nchi (CAF ranking), jambo ambalo huongeza au kudumisha nafasi ya Tanzania kuendelea kutoa timu nyingi na kunufaika na fursa za ushindani barani Afrika.
Kiuchumi, tathmini ya wazi inatupa picha ya fedha zinazopotea kwa sababu ya ubinafsi. Mchambuzi wa masuala ya soka na biashara ya michezo, Jemedari Said, mara kwa mara amekuwa akisisitiza kuwa thamani ya soka letu inapanda kimataifa pale tu timu zinapofika hatua za mbali za mashindano ya CAF. Hii inatafsiriwa kwenye ukweli rahisi: mchezaji wa Kitanzania anapouzwa kwenda nje ya nchi kwa dola elfu mia kadhaa kutokana na kuonekana kwenye televisheni za kimataifa, fedha hizo zinamnufaisha wakala, familia yake, na kukuza pato la taifa. Mjasiriamali wa chakula nje ya Uwanja wa Benjamin Mkapa hapati wateja kwa sababu mnunuzi ana kadi ya Yanga au Simba, bali anapata riziki kwa sababu uwanja umezalisha umati wa watu waliokuja kuangalia soka la kimataifa. Tunapowakalia koo wawakilishi wetu kwa sababu ya chuki za ligi ya ndani, tunakata matawi tunayokalia kiuchumi.
Kwenye safu ya kijiopolitiki, nguvu ya soft power inajengwa na mafanikio ya pamoja ya kitaifa. Wakati Simba au Yanga inapoenda ugenini nchini Misri au Afrika Kusini na kuandika historia, habari hizo zinaiweka Tanzania kwenye ramani ya kimataifa kama nchi inayoweza kushindana, na kufungua milango ya kidiplomasia na kiuwekezaji. Mkuu wa kitengo cha mawasiliano cha moja ya klabu hizo aliwahi kunukuliwa akisema: "Unapofika uwanja wa ugenini na kukuta maelfu ya watu wanakushangilia au kuheshimu uwezo wako, hawatamwita Mchezaji Fulani wa Yanga au Simba, watasema Watanzania wamekuja." Ni wazi kwa maneno mengine michezo ni silaha ya diplomasia isiyo na gharama kubwa ya kifedha kwa serikali, lakini inahitaji utayari wa wananchi wenyewe kutupa kando kofia za klabu zao na kuvaa kofia moja ya taifa.
Unaposikia viongozi wakitoa rai kama hii ya Dkt. Mwigulu, haipaswi kuchukuliwa kama porojo za kiofisi tu; ni wito wa kuokoa uchumi na mshikamano wa taifa letu kwenye ulingo wa kimataifa ambapo ushindani ni mkali na hauna huruma kwa waliogawanyika.

Post a Comment