Serikali Yakataza Utupaji Taka Hovyo, Yataka Utaratibu Madhubuti na Uwajibikaji kwa Kila Raia




Serikali imepiga marufuku utupaji taka hovyo na kusisitiza kuwa usafi wa mazingira si suala la hiari bali ni wajibu wa kisheria unaotakiwa kusimamiwa kwa umakini kuanzia ngazi ya vitongoji hadi mikoa. 

Agizo hilo limetolewa Dar es Salaam,Septemba 5, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira, Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, baada ya kuongoza zoezi la usafi katika Soko la Buguruni Jijini Dar es Salaam.

“Ni wajibu wa kila mwananchi, mfanyabiashara, mwekezaji, taasisi za Serikali, sekta binafsi, viongozi wa mitaa, wenye viwanda, watoa huduma za taka, taasisi za elimu na jamii kwa ujumla kuwa na utaratibu wa kufanya na kusimamia Usafi wa Mazingira katika maeneo yao.Hivyo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa tanzania inamtaka kila Mtanzania kushiriki katika usafi wa mazingira.” Amesema Mhe. Masauni.

Waziri Masauni alisisitiza katika hotuba yake kuwa viongozi wote wa Serikali za mitaa, wakuu wa wilaya na mikoa kuhakikisha wanaweka mfumo thabiti wa kusimamia agizo la kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kuwa siku rasmi ya usafi wa mazingira nchini.

“Tunakumbuka kuwa Serikali kupitia Mheshimiwa Rais akiwa Makamu wa Rais mwaka 2016 alitoa agizo kuwa kila Jumamosi ya mwisho ya mwezi kuwa siku ya usafi wa Mazingira Kitaifa," alisema Masauni kwa msisitizo.








Aidha Waziri Masauni alikumbusha kuwa  Ofisi ya Makamu wa Rais ilitoa ‘Enviromental Management (Designation of National Cleanliness Day) Guidelines , 2016,chini ya G.N.No.139 na kutaka viongozi wafuate Mwongozo huo ambao unaelekeza utekelezaji wa tamko la Serikali la kuitangaza kila jumamosi ya mwisho wa Mwezi kuwa siku ya usafi wa Mazingira Kitaifa.

Waziri Masauni ameeleza kuwa utupaji holela wa taka husababisha madhara makubwa kwa afya ya wananchi, kuharibu miundombinu na kuchangia kuziba kwa mifereji, hali inayosababisha magonjwa na kuongeza gharama za matibabu na usafi wa miji. 

Takwimu zinaonyesha kuwa ni asilimia 37 tu ya taka ngumu zinazozalishwa mijini ndizo zinazokusanywa ipasavyo, jambo linaloacha kiasi kikubwa cha taka kikiwa kimesambaa na kuharibu mandhari pamoja na kupunguza mvuto kwa watalii na wawekezaji.

Licha ya changamoto hiyo, serikali imesisitiza kuwa taka zinaweza kugeuzwa kuwa fursa kubwa ya kiuchumi kupitia urejelezaji, uzalishaji wa nishati, utengenezaji wa mboji na biashara ya kaboni, huku kukiwa na fursa ya uwekezaji inayokadiriwa kufikia shilingi bilioni 22 inayotokana na taka za plastiki, karatasi, taka za kielektroniki na betri chakavu. 

Kutokana na hali hiyo, serikali inawataka wananchi wote, wafanyabiashara, wamiliki wa viwanda, taasisi za serikali na sekta binafsi kuwajibika kikamilifu kwa kuhakikisha wanasimamia na kufanya usafi katika maeneo yao ili kulinda mazingira na afya za jamii.



No comments