Mikakati ya Serikali Kuimarisha Biashara ya Kaboni na Kulinda Maslahi ya Taifa
Serikali imeendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha Tanzania inatumia fursa ya biashara ya kaboni katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, huku ikihakikisha kuwa utekelezaji wa miradi inalinda maslahi ya taifa na kuleta manufaa kwa jamii.
Hatua hiyo imejadiliwa katika kikao kati ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Hamad Masauni na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji ambapo mawaziri hao wamekutana kuweka mikakati ya pamoja ya kuimarisha utekelezaji na usimamizi wa miradi ya biashara ya kaboni nchini.
Kikao hicho ni sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha fursa inayotokana na biashara ya kaboni inatumika kwa ufanisi katika kuhifadhi mazingira, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na wakati huo huo kuhakikisha rasilimali za nchi zinawanufaisha wananchi na taifa kwa ujumla.
Tanzania ni mwanachama wa mikataba mikuu ya kimataifa inayohusu mabadiliko ya tabianchi ikiwemo Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, Itifaki ya Kyoto na Makubaliano ya Paris, ambayo inalenga kuchukua hatua za kukabiliana na mabadiliko haya kupitia kupunguza uzalishaji wa gesijoto na kuimarisha uwezo wa kukabiliana na athari zake.
Katika kupunguza uzalishaji wa gesijoto, hatua zinaweza kuchukuliwa kupitia njia za asili, ikiwemo uhifadhi na uendelezaji wa misitu, usimamizi wa ardhi, kilimo na matumizi ya nishati safi, huku teknolojia za kisasa zikitumika katika sekta ya viwanda kupitia mifumo mbalimbali na uhifadhi, matumizi na utunzaji wa kaboni.
Kwa upande wa Tanzania, misitu ni miongoni mwa rasilimali muhimu katika kuhifadhi kaboni, hivyo kutoa fursa kubwa katika biashara hiyo inayotoa nafasi kwa nchi, taasisi na wawekezaji kutekeleza miradi inayolenga kupunguza au kuondoa gesijoto kutoka angahewa.
Dk Kijaji alisema Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais itaendelea kuimarisha ushirikiano katika kusimamia fursa hii muhimu kwa kuzingatia uhifadhi wa mazingira, maendeleo endelevu na maslahi ya taifa.
Kupitia hatua hizo, alisema Tanzania inalenga kujenga mazingira bora ya uwekezaji katika biashara ya kaboni, huku ikihakikisha kuwa fursa hiyo inakuwa chachu ya uhifadhi wa misitu na rasilimali nyingine za asili, kuongeza manufaa kwa jamii na kuchangia katika juhudi za kitaifa na kimataifa za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Post a Comment