Mama Fatma azikwa katika makaburi ya familia Mbweni
RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameongoza mamia ya waombolezaji kumzika mjane wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Fatuma Karume (97). Mama Fatma amezikwa katika makaburi ya familia Mbweni nje kidogo ya mji wa Unguja, Zanzibar.
Awali, mwili wa marehemu uliagwa nyumbani kwake Mbweni na kuswaliwa katika Msikiti wa Jamii Zenjibar uliopo Mazizini. Mufti wa Zanzibar, Saleh Kabi aliongoza sala ya kumuombea marehemu.
Rais Dk Samia Suluhu Hassan ametoa pole kwa Dk Mwinyi, Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari Machumu, imeeleza Rais Samia amesikitishwa na msiba huo.
Baada ya maziko, watoto wa marehemu, Rais mstaafu Amani Karume na Balozi Ali Karume, walikuwa wa kwanza kuweka mchanga katika kaburi la marehemu Wilaya ya Kaskazini B, Unguja.
Dk Mwinyi aliweka mchanga katika kaburi la marehemu na kufuatiwa na Makamu wa Kwanza wa Rais, Othman Masoud Othman na Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla.
Wengine ni viongozi wastaafu akiwemo Rais mstaafu wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein na Waziri Kiongozi mstaafu, Shamsi Vuai Nahodha.
Wengine walioshiriki na kuweka mchanga katika kaburi ni Jaji Mkuu, George Masaju na Naibu Spika wa Bunge, Daniel Sillo. Mama Fatuma alizaliwa Februari 2, 1929 eneo la Kaskazini B, Kijiji cha Bumbwini-Misufuni Mperani Mwisho wa Njia, Baba yake alifahamika kwa jina la Gulamhussein Jamal na mama yake ni Mwanaisha Binti Mbwana Ramadhani. Alifunga ndoa na Abeid Karume mwaka 1944, walijaliwa kupata watoto wawili, Rais mstaafu Amani Abeid Karume na Balozi Ali Karume.

Post a Comment