Jumuiya ya Madola Yapongeza Hatua za Maridhiano Tanzania
Kamati ya Mawaziri cha Jumuiya ya Madola wanaosimamia Utekelezaji wa
Maadili (CMAG) imetambua na kufurahishwa na ushirikiano mzuri ulioonyeshwa na
serikali ya Tanzania pamoja na hatua zilizochukuliwa kuwezesha maridhiano huko Zanzibar.
Kamati hiyo katika kikao chake cha 74 imesema hatua hizo zilizochukuliwa
ni msingi thabiti wa maendeleo zaidi ya kidemokrasia na kisiasa nchini Tanzania.
Kikao hicho
maalum kiliongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ulaya wa Malta, Mheshimiwa
Chris Fearne.
Katika kikao
hicho kilichofanyika mjini New York, viongozi na wawakilishi mbalimbali wa
ngazi za juu walihudhuria, wakiwemo Naibu Waziri Mkuu wa Samoa, Mheshimiwa
Mulipola Anarosa Ale Molioʻo, pamoja na mawaziri na wawakilishi maalum
kutoka nchi wanachama wa Antigua na Barbuda, Botswana, Canada, Grenada,
Malaysia, Mauritius, na Zambia.
Uwepo wa viongozi
hawa ulitoa fursa ya kufanya tathmini ya kina kuhusu masuala mbalimbali
yanayohusu nchi wanachama, ikiwemo Tanzania na Uganda, na kuweka mikakati ya
pamoja ya kuimarisha misingi ya demokrasia, utawala bora, na ushirikiano ndani
ya familia ya Jumuiya ya Madola.
Katika taarifa iliyotolewa kufuatia kikao chao maalum kilichofanyika
pembezoni mwa Mkuu wa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa mjini New York, pamoja
na kutambua maendeleo hayo chanya katika maeneo mbalimbali, CMAG ilisisitiza
haja ya kuendelea kufanya kazi ya ziada ili kuhakikisha kunakuwa na mchakato
jumuishi na wa wazi wa mazungumzo ya kisiasa ya vyama vingi, sambamba na
kulinda kwa dhati uhuru wa kiraia, kisiasa, na vyombo vya habari.
Kabla ya taarifa kamati hiyo ili ilipokea taarifa iliyowasilishwa kwa
kina na ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo, na Waziri wa Nchi, Ofisi
ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Prof. Palamagamba Kabudi.
CMAG imesifu utayari wa nchi ya Tanzania kushirikiana na Mjumbe Maalum
wa Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo katika kuimarisha misingi ya maridhiano na
maelewano ya kitaifa.
Hata hivyo walitilia mkazo maalum katika umuhimu wa kuzingatia taratibu
za kisheria zilizo wazi, za haki na kwa wakati unaofaa katika mashauri yote
yaliyopo wazi, pamoja na kuweka michakato inayoaminika ya uwajibikaji, utoaji
wa haki na fidia stahiki kwa wale wote waliothiriwa na matukio mbalimbali ya
nyuma, ili kuimarisha zaidi uaminifu na ustawi wa jamii.
Kufuatia tathmini hiyo ya kina, Jumuiya ya Madola imeihimiza serikali ya
Tanzania kupanga tarehe ya mapema kwa ajili ya ziara ya Katibu Mkuu wa Jumuiya
hiyo ili apate fursa ya kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Rais Samia
Suluhu Hassan pamoja na wadau wengine muhimu wa maendeleo na siasa nchini.
Kutokana na umuhimu wa mazungumzo hayo na hatua zinazoendelea
kuchukuliwa, kikao hicho kiliafikia makubaliano ya kuendelea kuweka Tanzania
kwenye ajenda yake rasmi ya ufuatiliaji, huku wakithibitisha utayari wa
kuendelea kutoa ushirikiano wa karibu na serikali katika kuhakikisha malengo ya
kidemokrasia, amani, na maendeleo endelevu yanatimizwa kwa maslahi mapana ya
wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kamati hiyo ya Mawaziri cha Jumuiya ya Madola inayosimamia Utekelezaji
wa Maadili (CMAG) ilianzishwa mwaka 1995 ili kuwa mlinzi na mtetezi wa maadili
na misingi ya kisiasa ya Jumuiya ya Madola.
Kamati hiyo inaundwa na mawaziri wa mambo ya nje kutoka nchi wanachama
nane zinazozunguka kanda mbalimbali kwa mfumo wa zamu, ikijumuisha pia waziri
wa mambo ya nje wa nchi iliyo Mwenyekiti Mkuu wa sasa wa Jumuiya hiyo ambaye ni
mwenyeji wa Mkutano uliopita wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM).
Kikao hicho cha 74 kiliitishwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya hiyo,
Mheshimiwa Shirley Botchwey.

Post a Comment