Bandari ya Dar es Salaam ni Lango Kuu la Biashara na Uchumi wa Kikanda’
Bandari ya Dar es Salaam inazidi kuimarika kama lango kuu la kimkakati
linalounganisha Afrika na masoko ya dunia, huku ikichochea ukuaji wa uchumi wa
kikanda katika kipindi hiki ambacho mabadiliko ya minyororo ya ugavi duniani
yanabadilisha mtazamo wa kibiashara.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa
Kitengo cha Mashirika Makubwa wa Benki ya Absa Tanzania, Nellyana Mmanyi,
wakati akizungumza katika mkutano wa GTR East Africa 2026 uliofanyika jijini
Nairobi, Kenya, ukikutanisha wadau wa biashara, fedha, na uwekezaji.
Mmanyi alieleza kuwa mazingira yanayobadilika ya uchumi wa dunia yanaipa
Afrika Mashariki fursa ya kipekee ya kuwa kitovu cha uzalishaji na kiunganishi
cha kimkakati, akisisitiza kuwa eneo hilo linanufaika na msimamo wake wa
kijiografia na uhusiano thabiti na Mashariki ya Kati na Asia.
Alibainisha kuwa bandari hiyo inafanya kazi kubwa ya kuhudumia biashara
ya Tanzania pamoja na nchi jirani zisizo na bandari, zikiwemo Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zambia, Uganda, na Rwanda, huku Ukanda wa Kati ukiendelea
kuimarishwa kama njia kuu na muhimu ya usafirishaji wa mizigo ya kikanda.
Licha ya fursa hizo kubwa, Mmanyi alionya kuwa wafanyabiashara bado
wanakabiliwa na vikwazo mbalimbali vya kuvuka mipaka, ikiwemo ucheleweshaji wa
forodha, mifumo isiyo na ufanisi ya usafirishaji, tofauti za kanuni, na
changamoto za miundombinu zinazoongeza gharama na muda.
Alisisitiza kuwa ili Eneo Huru la Biashara Barani Afrika (AfCFTA) liwe
na tija ya dhati, linapaswa kutoka kwenye ahadi za kisera na kuwa utekelezaji
wa vitendo kwa kuondoa vikwazo visivyo vya ushuru, huku benki zikiendelea kutoa
ufadhili jumuishi na huduma za kifedha kusaidia kampuni kukabili changamoto za
masoko ya kikanda.
mwisho
Post a Comment